Raia wa Guinea wanatarajiwa kupiga kura Jumapili katika uchaguzi wa kwanza wa rais tangu jeshi lichukue madaraka kupitia mapinduzi ya mwaka 2021, huku wachambuzi wakitabiri ushindi wa kiongozi wa junta, Jenerali Mamadi Doumbouya.
Guinea ni miongoni mwa mataifa 10 ya Afrika ambako wanajeshi wamechukua mamlaka tangu 2020, huku baadhi yao baadaye wakishinda chaguzi baada ya kuchelewesha kurejea kwa utawala wa kiraia. Tangu kumuondoa madarakani Rais Alpha Condé miaka minne iliyopita, wakosoaji wanasema Doumbouya amedhibiti vikali upinzani na sauti za ukosoaji, hali iliyomwacha bila mpinzani mwenye nguvu kuelekea muhula wa miaka saba.
Licha ya kuwa na utajiri mkubwa wa rasilimali za madini — ikiwemo kuwa msafirishaji mkubwa zaidi duniani wa bauxite inayotumika kutengeneza alumini — zaidi ya nusu ya watu milioni 15 wa Guinea wanakabiliwa na viwango visivyokuwa vya kawaida vya umaskini na uhaba wa chakula, kwa mujibu wa Shirika la Chakula Duniani, WFP.
Takribani wapiga kura milioni 6.7 waliojiandikisha wanatarajiwa kupiga kura katika vituo karibu 24,000 kote nchini, huku matokeo yakitarajiwa kutangazwa ndani ya saa 48. Ikiwa hakuna mgombea atakayepata zaidi ya nusu ya kura, duru ya pili itafanyika. Jumuiya ya kikanda ya Afrika Magharibi, ECOWAS, imetuma ujumbe wa waangalizi wa uchaguzi.
Upinzani dhaifu
Jumla ya wagombea tisa wanashiriki uchaguzi huo. Mpinzani wa karibu zaidi wa Doumbouya ni Yero Baldé, mgombea asiyejulikana sana kutoka chama cha Democratic Front of Guinea, aliyewahi kuwa waziri wa elimu chini ya Condé. Baldé ameahidi mageuzi ya utawala, vita dhidi ya rushwa na kukuza uchumi.
Wagombea wawili wa upinzani — aliyewahi kuwa waziri mkuu Lansana Kouyaté na aliyekuwa waziri Ousmane Kaba — waliondolewa kwa sababu za kiufundi, huku vigogo wa muda mrefu wa upinzani Cellou Dalein Diallo na Sidya Touré wakilazimika kuishi uhamishoni.
Mashaka kuhusu uhalali wa kura
Katika mji mkuu Conakry, maoni yamegawanyika kuhusu kama uchaguzi huo utaakisi matakwa ya wananchi. Uchaguzi unafanyika chini ya katiba mpya iliyoondoa marufuku ya viongozi wa kijeshi kugombea urais na kuongeza muda wa muhula kutoka miaka mitano hadi saba. Katiba hiyo iliidhinishwa Septemba kupitia kura ya maoni ambayo vyama vya upinzani vilihimiza wananchi kuisusia.
Alioune Tine, mwanzilishi wa Afrikajom Center, amesema hakuna matumaini makubwa kuwa kura hiyo itaashiria kurejea kwa demokrasia ya kweli. Alisema uchaguzi unafanyika bila viongozi wakuu wa upinzani na katika mazingira ambayo nafasi ya kiraia imebanwa sana, akiongeza kuwa lengo kuu ni kuhalalisha mamlaka ya Doumbouya.
Mmiliki wa mgahawa mjini Conakry, Mamadou Bhoye Diallo, amesema hatapiga kura, akitaja uchaguzi huo kuwa mzaha. Alisema pale mgombea anapokuwa pia msimamizi wa mchakato, haiwezekani kutarajia haki, huku vyama vikuu vikiwa pembeni na viongozi wao uhamishoni.
Wanaharakati na mashirika ya haki za binadamu wanasema tangu mapinduzi, Guinea imeshuhudia viongozi wa asasi za kiraia kunyamazishwa, wakosoaji kutekwa na vyombo vya habari kudhibitiwa. Mwaka jana, serikali ilivunja zaidi ya vyama 50 vya siasa, ikidai ilikuwa inasafisha mfumo wa kisiasa.
Mwitikio mseto kwa uchaguzi wa kwanza tangu mapinduzi
Hata hivyo, Doumbouya anaungwa mkono na sehemu ya wananchi waliovutiwa na ahadi zake za kuleta ustawi wa kiuchumi. Kampeni yake imejikita katika miradi mikubwa ya miundombinu na mageuzi yaliyoanzishwa tangu achukue madaraka.
Mwanafunzi wa shule ya sekondari, Mamadama Touré, aliyevalia fulana yenye picha ya Doumbouya, alisema kiongozi huyo ni mtetezi wa vijana, akitaja programu za mafunzo ya ujuzi wa kidijitali kama mafanikio makubwa.
Miongoni mwa miradi mikubwa ya utawala wa kijeshi ni mradi wa uchimbaji madini wa Simandou, unaomilikiwa kwa asilimia 75 na Wachina, katika hifadhi kubwa zaidi duniani ya madini ya chuma. Mradi huo ulianza uzalishaji mwezi uliopita baada ya kucheleweshwa kwa miongo kadhaa, na serikali inasema utakuwa nguzo ya mageuzi ya uchumi.
Serikali pia imesema mpango wa maendeleo wa kitaifa unaohusishwa na Simandou unalenga kuunda makumi ya maelfu ya ajira na kubadilisha uchumi kupitia uwekezaji katika kilimo, elimu, usafirishaji, teknolojia na afya.
Kwa kampeni zenye mikutano mikubwa na uangalizi mpana wa vyombo vya habari, pamoja na msaada wa rasilimali za serikali, Doumbouya ametawala mazingira ya kisiasa, akiwapa wapinzani wake wenye rasilimali ndogo changamoto kubwa kuelekea siku ya kura.