BAADA ya jana kupigwa mechi mbili za raundi ya 12 za Ligi ya Championship, msako mwingine wa kuwania pointi tatu muhimu unaendelea leo Jumamosi na kesho Jumapili, huku ushindani kwa kila timu ukizidi kuongezeka pia kila uchao.

Vinara wa ligi hiyo, Geita Gold iliyolazimishwa sare ya bao 1-1, mechi iliyopita dhidi ya Kagera Sugar iliyo nafasi ya pili, itakuwa kwenye Uwanja wa Nyankumbu Geita kucheza na KenGold, yenye kumbukumbu ya kuchapwa mabao 2-1 na Songea United.

Geita iliyoshuka daraja msimu wa 2023-2024, msimu wa 2024-2025 wa Ligi ya Championship ilimaliza nafasi ya nne na pointi 56, chini ya aliyekuwa Kocha Mkuu, Mohamed Muya na kushindwa kupanda Ligi Kuu Bara, baada ya kufeli mechi za ‘Play-Off’.

Timu hiyo ilicheza ‘Play-Off’ ya kupanda Ligi Kuu Bara dhidi ya Stand United ‘Chama la Wana’ iliyomaliza nafasi ya tatu na pointi 61 na kushuhudia ikiondoshwa kwa jumla ya mabao 4-2, baada ya sare nyumbani ya 2-2 kisha kuchapwa ugenini 2-0.

CHAMPI 01

Hata hivyo, msimu huu timu hiyo imeanza vyema chini ya Kocha, Zubery Katwila baada ya kushinda mechi tisa na kutoka sare miwili kati ya 11, iliyocheza hadi sasa, huku safu ya ushambuliaji ya kikosi hicho ikifunga mabao 22 na kuruhusu manne.

Kwa upande wa KenGold, baada ya msimu bora wa 2023-2024, ilipotwaa ubingwa wa Ligi ya Championship na kucheza Ligi Kuu Bara msimu wa 2024-2025, wengi walitarajia ingefanya vizuri, ingawa mambo yalikuwa tofauti na kurejea ilikotoka.

Licha ya kiwango bora ilichokionyesha Championship, ila KenGold ilishindwa kumudu presha za Ligi Kuu na kuburuza mkiani na pointi 16, ikishinda mechi tatu, sare saba na kupoteza 20, ikiungana na Kagera Sugar iliyomaliza ya 15 na pointi 23.

CHAMPI 02

Kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, mabingwa wa First League msimu wa 2024-2025, Gunners iliyochapwa bao 1-0, dhidi ya Stand United, itaikaribisha Mbeya Kwanza ambayo kwa sasa ina rekodi bora ya kushinda mechi nane mfululizo zilizopita.

Mechi ya mwisho kwa leo Jumamosi itapigwa kwenye Kituo cha Ufundi cha TFF, Kigamboni na Barberian zamani Kiluvya United inayoburuza mkiani itacheza na Hausung ya Njombe, huku timu zote zikiwa zimekusanya pointi tatu kwa kila mmoja.

Barberian iliyochapwa mabao 2-0 na Transit Camp, ndiyo timu hadi sasa katika Championship ambayo haijashinda, imecheza mechi 11, imeshachapwa nane na kutoka sare tatu, ikifunga mabao matano na kuruhusu 21.

CHAMPI 03

Kwa upande wa Hausung inayoshika nafasi ya 15 na pointi tatu pia, imecheza mechi 11, imeshinda mmoja na kuchapwa 10, huku safu ya ushambuliaji ya timu hiyo ikifunga mabao manane na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 22.

Ligi hiyo itaendelea tena kesho Jumapili kwa mechi tatu kupigwa na Kagera Sugar baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Geita Gold, itakuwa kwenye Uwanja wa Kaitaba Bukoba, mkoani Kagera dhidhi ya Songea United iliyoichapa KenGold mabao 2-1.

Kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha, wenyeji TMA iliyotoka kuchapwa bao 1-0 katika mechi ya ‘Arusha Monduli Derby’, dhidi ya Mbuni, itaikaribisha maafande wa Polisi Tanzania yenye kumbukumbu ya kuichapa African Sports mabao 3-0.

CHAMPI 04

Ushindi huo wa Polisi wa mabao 3-0, dhidi ya African Sports, ulikuwa ni wa kwanza kwa timu hiyo inayofundishwa na Mbwana Makata, ilishacheza mechi saba mfululizo bila ya kushinda, baada ya kuchapwa miwili na kutoka sare mitano tu.

Timu hiyo msimu uliopita wa 2024-2025, haukuwa mzuri sana baada ya kumaliza nafasi ya 10, katika Ligi ya Championship na pointi 33, ikishinda mechi nane, sare tisa na kupoteza 13 na safu ya ushambuliaji ilifunga mabao 44 na kuruhusu 33.

Kikosi hicho kinapambana ili kurejea tena Ligi Kuu Bara baada ya kushuka daraja msimu wa 2022-2023, kilipomaliza nafasi ya 15 na pointi zake 25, baada ya kushinda mechi sita, sare saba na kupoteza 17, kikifunga mabao 25 na kuruhusu 54.

CHAMPI 05

Mechi ya mwisho na ya kuhitimisha raundi ya 12, itapigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga na African Sports iliyoshuka daraja kutoka Ligi Kuu hadi Championship msimu wa 2015-2016, itakuwa na kibarua cha kupambana dhidi ya Mbuni.

Kocha wa Mbuni, Leonard Budeba, alisema ushindi wa mechi iliyopita umeamsha morali ya wachezaji wa timu hiyo baada ya mwenendo usioridhisha, japo bado wana kazi kubwa ya kufanya kutokana na ushindani wa wapinzani wao walio nafasi za juu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *