MRADI wa Eco-School ni muhimu katika kuimarisha elimu ya mazingira na maendeleo endelevu kwa wanafunzi, jamii na taifa kwa ujumla. Mradi huu unawawezesha watoto kujifunza kwa vitendo, kukuza uongozi na kushiriki moja kwa moja katika uhifadhi wa mazingira na rasilimali asilia.
Moja ya manufaa makubwa ya mradi huu kwa kizazi cha sasa ni kuimarisha elimu kwa vitendo. Kupitia Eco-School, wanafunzi hawajifunzi kwa nadharia pekee, bali hushiriki shughuli halisi kama kilimo cha bustani za shule, utunzaji wa misitu na utekelezaji wa miradi ya nishati safi.
Njia hii huwajengea uelewa mpana na wa kudumu kuhusu umuhimu wa mazingira katika maisha ya kila siku. Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wanaposhiriki katika miradi ya kijamii inayohusiana na mazingira, hujengewa misingi ya uongozi bora na maono ya kijani.
Kwa mantiki hiyo, mradi wa Eco-School umebeba dhamana ya kumlea mtoto katika misingi ya utunzaji wa mazingira tangu akiwa mdogo, ili aelewe wajibu wake katika kulinda mazingira kwa manufaa ya sasa na ya baadaye. Kupitia mradi huu, wanafunzi hujifunza mbinu mbalimbali za kiikolojia kama matumizi endelevu ya rasilimali, uhifadhi wa nishati, upandaji miti na kudumisha usafi wa mazingira.
Aidha, hujifunza kwa vitendo kuhusu uendelevu wa mazingira, uzalishaji wa chakula bora kupitia kilimo hai, pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa za nishati safi kama nishati ya jua. Shule zinazotekeleza Eco-School hushirikishwa pia katika mipango ya kupunguza uchafuzi wa mazingira, kuongeza uelewa kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi na kutekeleza miradi midogo midogo ikiwemo bustani za shule, vituo vya kuchakata taka na matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira.
Hatua hizi huandaa wanafunzi kuwa mabalozi wa mazingira katika jamii zao. Mwaka 2025, shule 41 za msingi na sekondari, kwa mujibu wa Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) linalosimamia utekelezaji wa mradi huu, zimekidhi vigezo saba vya kupatiwa bendera ya kimataifa ya kijani kama utambuzi wa kazi nzuri iliyofanywa.
Shule hizo zinatoka katika wilaya za Kilosa, Mvomero, Morogoro na Mufindi mkoani Iringa. Utekelezaji wa mradi huu umekuwa nyenzo muhimu katika kusaidia serikali kuboresha elimu, kuongeza stadi za maisha na ujasiriamali kwa wanafunzi, sambamba na kujenga utamaduni wa kujitegemea. Shule zimefanikiwa kuzalisha mazao mbalimbali yakiwemo matunda na mboga, kuyauza katika masoko ya ndani na hivyo kuongeza kipato cha shule na hata kuwajengea wanafunzi ujuzi wa kujitegemea wanaporejea nyumbani.
Kwa msingi huo, wanafunzi wananufaika kiuchumi kwa kuanzisha miradi yao binafsi wakiwa nyumbani, ikiwemo bustani za mboga, kilimo cha migomba na matumizi ya mbolea ya asili wanayoitengeneza wenyewe bila kemikali. SOMA: Waomba mazingira bora zaidi elimu jumuishi
Hali hii husaidia kupunguza gharama za maisha kwa familia zao. Ni wito wangu kwa viongozi wa shule husika na nyinginezo kuanzisha na kuimarisha mikakati endelevu inayotumia mbinu shirikishi za utunzaji wa mazingira kwa wanafunzi. Hatua hii itajenga kizazi chenye uwezo wa kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na chenye ujuzi wa kuanzisha miradi ya kujipatia kipato.
Nina imani kuwa endapo mpango huu utawekewa mkazo zaidi shuleni, utaleta faida kubwa si kwa shule pekee bali pia kwa wanafunzi wanapokuwa shuleni na hata baada ya kumaliza masomo yao, kwa kuwajengea uwezo wa kuendesha miradi itakayowaingizia kipato na kupunguza mzigo wa gharama za maisha kwa wazazi wao.
