s

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 2

Tanzania na Uganda wamelazimika kugawana alama baada ya kutoka sare ya 1–1 katika dabi ya Afrika Mashariki ya kwenye michuano ya AFCON 2025, matokeo ambayo yanaacha hatima ya timu zote mbili ikining’inia kuelekea michezo ya mwisho ya kundi.

Kipindi cha kwanza kilikuwa chini ya udhibiti wa Uganda, waliocheza kwa kujiamini na kuwabana Tanzania katika nusu yao ya uwanja. Cranes walionekana kuwa na mpango mzuri wa kumiliki mpira na kushambulia kupitia mipira ya juu, lakini walikosa umakini katika eneo la mwisho.

Kipindi cha pili kilipoanza, Tanzania walibadilika. Ndani ya dakika 10 za mwanzo, Taifa Stars waliongeza kasi na kuanza kuucheza mpira kwenye nusu ya Uganda, shinikizo lililozaa penati ambayo Simon Msuva aliitumia vyema kuiweka Tanzania mbele.

Hata hivyo, dakika 15 za mwisho waganda waliongeza nguvu na kuanza kuingia kwa kasi katika eneo la Tanzania, hali iliyowalipa walipopata bao la kusawazisha kupitia Uche Ikpeazu.

Dakika za mwisho za mchezo zilikuwa za aina yake. Uganda walipata nafasi ya kuondoka na ushindi baada ya kuzawadia penati dakika ya 89, lakini Allan Okello alipaisha kwaju huo.

Dakika moja baadaye, Tanzania nao walikaribia kupata bao la ushindi. Krosi ya Mohamed Hussein haikuokolewa vizuri na kipa wa Uganda, Denis Onyango, na mpira ukamkuta Charles M’Mombwa akiwa kwenye nafasi ya wazi, lakini mshambuliaji huyo alishindwa kuumalizia, akipoteza nafasi ambayo ingebadilisha hatima ya dabi hiyo, hasa kwa Tanzania.

Filimbi ya mwisho ikapulizwa huku sare ya 1–1 ikibaki kuwa matokeo rasmi, kila upande ukiondoka na hisia za kujilaumu kwa nafasi walizokosa, na kufanya nafasi ya kufuzu 15 bora kuwa shakani. Tanzania itamaliza kwa kumenyana na Tunisia na Uganda itakumbana na Nigeria.

Uganda waliiingia kwenye mechi hii wakiwa na uzito mkubwa wa historia ya AFCON. Kipigo cha 3–1 dhidi ya Tunisia kilikuwa ni cha 17 kwa Cranes katika mechi 24 walizowahi kucheza AFCON. Pia kiliendeleza rekodi mbaya ya Uganda ya kupoteza michezo ya ufunguzi, wakifanya hivyo mara tano katika nane walizowahi kushiriki.

Tanzania imepoteza kila mchezo wa ufunguzi wa michuano ya AFCON, Uganda wao imepoteza kwenye michezo ya pili ya makundi. Tangu mfumo wa makundi ulipoanzishwa mwaka 1968, Uganda hawajawahi kushinda mchezo wa pili wa kundi. Wamepoteza mara nne na kutoa sare mara mbili. Mara tatu waliwahi kupoteza michezo miwili ya kwanza ya kundi mwaka 1962, 1968 na 1976 na mara zote waliondolewa mapema.

Ndugu wametoshana nguvu, macho sasa katika michezo yao ya mwisho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *