Songwe. Shirika la Ushirikiano wa Maendeleo la Kimataifa la Korea (Koica) na Shirika la Good Neighbors Tanzania sambamba na wadau wakiwamo wa sekta ya kilimo cha mahindi Mkoani Songwe, wamekubaliana vipaumbele vya mwaka 2026, vinavyoenda kutekelezwa.

Hayo yamejiri leo katika warsha Mbali na mambo mengine, imezungumzia utekelezaji wa Mradi wa Mahindi Songwe unaofadhiliwa na Koica.

Vipaumbele vilivyotajwa kwa mwaka 2026 ni pamoja na kuimarisha huduma za ushauri wa kilimo kwa wakulima, kupanua kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi, kuboresha upatikanaji wa mbegu bora na kuimarisha ushirikiano kati ya wadau katika ngazi ya mkoa na wilaya.

Lengo kuu limeelezwa ni kutaka kuendelea kuimarisha uhakika wa chakula na kukuza kipato cha wakulima wadogo.

Taasisi zilizoshiriki warsha hiyo ni pamoja na ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari), Wakala wa Mbegu za Kilimo (Asa), Taasisi ya Uthibitishaji Mbegu Tanzania (TOSCI), vyama vya ushirika (AMCOS) na wadau wa maendeleo.

Akizungumza katika kikao hicho kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Farida Mgomi amesema mradi huo una lengo la kuboresha usalama wa chakula na kuongeza kipato cha wakulima kupitia mtandao wa vyama vya ushirika (AMCOS), hususan katika Halmashauri ya Wilaya ya Ileje na Halmashauri ya Mji wa Tunduma.

Mgomi amesema mradi huo ni fursa muhimu kwa wakulima wa mahindi katika kuongeza uzalishaji na hivyo kuchangia kukuza uchumi wa wananchi na mkoa kwa ujumla.

“Kwa niaba ya Serikali, natia pongezi za dhati kwa wafadhili wa mradi huu chini ya Koica pamoja na Shirika la Good Neighbors Tanzania kwa kuona umuhimu wa kuwekeza katika sekta ya kilimo, sekta ambayo inatoa ajira kwa zaidi ya asilimia 75 ya wananchi wa Mkoa wa Songwe,” amesema Mgomi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Good Neighbors Tanzania, Il Sun Jung amesema mradi huo umejikita katika kuunganisha wakulima, taasisi na masoko ili kujenga msingi wa maendeleo endelevu yatakayodumu hata baada ya mradi kukamilika.

“Kwa kuunganisha wakulima, taasisi na masoko, tunaweka msingi wa athari za muda mrefu zitakazodumu hata baada ya mradi kukamilika,” amesema Jung.

Amesema wadau waliokutana katika warsha hiyo wamethibitisha dhamira yao ya ushirikiano endelevu, huku wakibainisha kuwa mradi wa Koica ni mfano halisi wa maendeleo ya kilimo jumuishi yanayolenga kuboresha maisha ya wakulima wadogo mkoani Songwe.

Mradi wa Mahindi Songwe ulianza Machi 2025 na unatarajiwa kukamilika Desemba 2027, ukiwa na malengo ya kuboresha mavuno ya mahindi, kuimarisha mtandao wa vyama vya ushirika (AMCOS) na kuongeza kipato cha wakulima wadogo.

Jung amesema unawalenga wanachama wa vyama vya ushirika (AMCOS) pamoja na wakulima wadogo katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma na Wilaya ya Ileje.

Lengo lingine ni kuongeza usalama wa kipato kwa wakulima kupitia mtandao wa maghala na kuimarisha mnyororo wa thamani wa zao la mahindi.

Wakulima na maofisa wa mradi wamebainisha mafanikio yaliyopatikana mwaka huu, yakiwamo kuongezeka kwa mavuno ya mahindi, upatikanaji wa mbegu bora, matumizi ya mbinu za kisasa za kilimo na kuongezeka kwa ujuzi wa wakulima kupitia mafunzo na mashamba darasa.

Aidha, amesema wamepiga hatua kwenye maendeleo hususan kati ya wakulima, vyama vya ushirika na masoko, kupitia mitandao ya maghala ya shirikisho, hatua inayotarajiwa kuongeza tija na ushindani wa zao la mahindi mkoani Songwe.

Warsha hiyo imehudhiriwa pia na Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe, Dk Hawasi Haule, pamoja na Wakuu wa Wilaya za Ileje na Momba.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *