MBEYA: Hatua ya Bodi ya Maji Bonde la Rufiji kupitia Mradi wa NBS–USANGU kuanza urejeshaji wa mito iliyopoteza mwelekeo wake wa asili imeanza kuandika ukurasa mpya wa matumaini kwa wananchi wa Bonde la Usangu, wilayani Mbarali mkoani Mbeya.

Kwa miaka mingi, mito kadhaa katika bonde hilo ilikuwa imejaa mchanga, kupoteza mikondo yake na mingine kukauka kabisa, hali iliyosababisha uhaba wa maji, kushuka kwa uzalishaji wa kilimo na kuibua migogoro ya matumizi ya rasilimali za maji.

Akizungumza baada ya ziara ya wajumbe wa Kamati ya Uongozi wa Mradi wa NBS–USANGU waliotembelea na kujionea kazi ya urejeshaji wa Mto Mlowo, Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Rufiji, Mhandisi David Munkyala, alisema zoezi hilo ni sehemu ya mkakati mpana wa kurejesha ikolojia ya mito na kulinda rasilimali za maji kwa manufaa ya wananchi wa sasa na vizazi vijavyo.

Alisema kwa muda mrefu shughuli za kibinadamu pamoja na mmomonyoko wa ardhi zilisababisha mito mingi kupoteza mwelekeo wake wa asili, jambo lililoathiri moja kwa moja maisha ya wananchi wanaotegemea kilimo na mifugo.

“Kupitia mradi huu unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia Serikali ya Japan, tunarejesha mifumo ya asili ya mito ili maji yarudi kwenye mikondo yake sahihi. Hii si tu inalinda mazingira, bali pia inaleta suluhisho la kudumu kwa changamoto ya maji,” alisema Mhandisi Munkyala.

Aliongeza kuwa urejeshaji wa Mto Mlowo utaongeza upatikanaji wa maji ya uhakika kwa matumizi ya kilimo na mifugo, sambamba na kupunguza migogoro ya muda mrefu ya matumizi ya rasilimali za maji katika jamii.

“Tunataka wakulima wapate maji mashambani, mifugo ipate maji bila kuharibu vyanzo, na mazingira yahifadhiwe. Haya ndiyo malengo makuu ya Mradi wa NBS–USANGU,” alisisitiza.

Mhandisi Munkyala alibainisha kuwa mafanikio ya mradi huo yanategemea kwa kiasi kikubwa ushiriki wa wananchi na wadau wengine wakiwemo serikali za mitaa na taasisi mbalimbali.

“Mradi huu ni wa wananchi. Bila ushiriki wao katika kulinda maeneo yaliyorejeshwa na miundombinu iliyowekwa, jitihada hizi haziwezi kudumu,” alisema.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa NBS–USANGU kutoka Bodi ya Maji Bonde la Rufiji, David Muginya, alisema mradi huo umebuniwa kwa kutumia suluhisho la asili (Nature-Based Solutions) linalolenga kurejesha uwiano kati ya shughuli za binadamu na mazingira.

Alisema mradi huo unagusa moja kwa moja maisha ya wananchi kwa kuimarisha uzalishaji wa kilimo, kuongeza usalama wa chakula na kuinua kipato cha kaya, huku ukipunguza athari za ukame na mafuriko yasiyotabirika.

“Tayari vijiji vingi vinavyopakana na mito katika Bonde la Usangu vinaanza kuona matokeo chanya. Maji yanaanza kupatikana, mashamba yanaanza kurejea kwenye uzalishaji, na matumaini mapya yanachipua,” alisema Muginya.

Wajumbe wa Kamati ya Uongozi wa Mradi wa NBS–USANGU akiwemo Said Juma na Simon Kitereja walieleza kuridhishwa kwao na hatua iliyofikiwa baada ya kujionea urejeshaji wa Mto Mlowo, wakisema mradi huo ni mfano wa matumizi sahihi ya fedha za mradi na dhamira ya dhati ya kulinda rasilimali za maji.

Kwa upande wa wananchi, Hamis Mwatenga, mkazi wa Kijiji cha Mwatenga, Kata ya Mahongole, alisema urejeshaji wa mto umeanza kuondoa hofu waliyoishi nayo kwa miaka mingi.

“Awali tulikuwa tunahangaika sana kupata maji mashambani. Mto ulikuwa umepotea kabisa, lakini sasa tunaona mabadiliko. Hii inatupa matumaini mapya,” alisema.

Naye Omary Makolo, mkazi wa Kijiji cha Ilaji, alisema mradi huo umeongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa mazingira na kulinda vyanzo vya maji.

“Mradi huu umetufundisha kuwa kulinda mazingira ni kujilinda sisi wenyewe na maisha yetu ya baadaye,” alisema.
Utekelezaji wa Mradi wa NBS–USANGU ni matokeo ya jitihada za Bodi ya Maji Bonde la Rufiji kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, kulinda rasilimali za maji, kurejesha mazingira na kuboresha maisha ya wananchi katika Bonde la Usangu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *