SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), limeweka masharti mapya kwa makocha ambao wataongoza timu katika mashindano tofauti yaliyo chini ya shirikisho hilo, uamuzi ambao hapana shaka utagusa moja kwa moja mashindano ya ndani hapa Tanzania.

Kuanzia hivi sasa na kuendelea, CAF imeweka sharti la Kocha Msaidizi kuwa na leseni Daraja A au Pro ya shirikisho hilo au leseni Daraja la Pro kutoka shirikisho la bara lingine.

Uamuzi huo unaonekana usingeweza kuziathiri klabu nne za Tanzania ambazo zilishiriki mashindano ya Klabu Afrika msimu huu, Yanga, Simba, Azam na Singida Black Stars kwani zote zina makocha wakuu na wasaidizi wanaokidhi vigezo hivyo vipya.

Hata hivyo, kama masharti hayo yangetolewa mwanzoni mwa msimu, aliyekuwa Kocha wa Simba, Dimitar Pantev asingeruhusiwa kuwepo katika benchi la ufundi kwani ana leseni A ya Umoja wa Vyama vya Mpira wa Miguu Ulaya (UEFA).

Ipo hivi; Awali, kocha msaidizi aliruhusiwa kukaa kwenye benchi akiwa na leseni daraja B ya CAF au A ya mashirikisho mengine kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Kombe la Shirikisho Afrika au mashindano ya timu za taifa za wakubwa kwa upande wa wanaume.

Kwa upande wa mashindano ya timu za taifa za wanawake za wakubwa na mashindano ya klabu za wanawake Afrika, masharti ya CAF ni kama ilivyo kwa wanaume ingawa kwa kocha msaidizi anaweza kuwa na leseni B ya shirikisho hilo ingawa kwa mashirikisho mengine ni lazima iwe leseni ya Pro.

Timu za vijana za umri wote kwa wanaume zinapaswa kufundishwa na makocha wenye leseni A ya CAF wasaidizi wawe na B huku wakitakiwa kuwa na leseni ya daraja la Pro ikiwa wanatokea katika mashirikisho mengine.

Makocha wanaozifundisha timu zote za vijana za wanawake wanapaswa kuwa na angalau leseni daraja B ya CAF au A kutoka mashirikisho mengine na upande wa wasaidizi wawe na angalau C ya CAF na ya mashirikisho mengine inapaswa angalau kuwa daraja A.

Sharti lingine ambalo CAF imeliweka ni timu zinazoshiriki mashindano ya wanawake ya CAF, kuhakikisha angalau mmojawapo kati ya Kocha Mkuu au Msaidizi anakuwa ni mwanamke tofauti na zamani ambapo iiruhusiwa wawe hata wanaume tupu.

Kwa upande mwingine, uwepo wa Kocha Msaidizi Edna Lema katika kikosi cha timu ya taifa ya wanawake Tanzania, Twiga Stars, kunaifanya timu hiyo iwe salama katika Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON 2026) zitakazofanyika Machi 17, 2026 hadi Aprili 3, 2026 huko Morocco, kwa vile kocha huyo ana leseni daraja A ya CAF.

Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Oscar Mirambo, amesema masharti hayo yataingizwa katika kanuni za mashindano ya hapa nchini siku za usoni lakini kabla ya hilo kufanyika lazima wafanye maandalizi ya kiuwezeshaji makocha.

“Kila tunachokifanya kina athari ya moja kwa moja kutoka CAF na FIFA. Ikiwa hivyo maana yake tunatakiwa kufanyia kazi kile ambacho kinafanywa na wa juu yetu kwa maana hiyo nchi, vyama na mashirikisho wanachama tunapaswa kuendana na kinachotokea.

“Litakuwa jambo la hatari kwa vyama na mashirikisho wanachama ziko tofauti na vigezo vya CAF. Lakini hatuwezi kuingiza tu maelekezo hayo kwenye kanuni zetu kabla ya kuwajengea watu wetu uwezo. Tunatakiwa tujenge uwezo ili pale tunapoamua kuingiza kwenye kanuni zetu, tuwe tunaweza kumudu mahitaji,” amesema Mirambo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *