BEKI wa kati wa Geita Gold, Ally Ally, amesema ubora na upana wa kikosi hicho ndio sababu ya kufanya vizuri msimu huu, licha ya kukiri ushindani umekuwa mkubwa, kutokana na timu zote kupigania kumaliza ndani ya nafasi mbili za juu kwenye msimamo.

Nyota huyo aliyejiunga na kikosi hicho akitokea Bigman aliyoongoza kwa kuifungia mabao matano msimu uliopita, amesema uwepo wa wachezaji wengi bora katika kila eneo unachangia kufanya vizuri kwa Geita, ingawa wanapaswa kupambana zaidi.

“Tunaishi familia kuanzia viongozi, wachezaji na hata benchi la ufundi, hii inatusaidia sana kwa sababu kila anayepewa nafasi ya kucheza anapambana ili tu apangwe tena, kwetu ni jambo nzuri kutokana na malengo tuliyojiwekea,” amesema Ally.

Nyota huyo aliyewika na timu mbalimbali zikiwamo, KVZ, Yanga, Stand United na KMC, amesema licha ya ushindani mkubwa wa wapinzani wao ila hilo kwao haliwatishi, kwa sababu wanachofanya ni kuhakikisha kila mechi wanayocheza wanafanya vizuri.

Geita iliyoshuka daraja msimu wa 2023-2024, msimu huu wa 2025-2026, inaongoza katika msimamo na pointi 30, baada ya timu hiyo kucheza mechi 12, ambapo kati ya hizo imeshinda tisa na kutoka sare mitatu tu, ikifunga mabao 24 na kuruhusu sita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *