KOCHA mpya wa Simba, Steve Barker ametua nchini alfajiri ya jana na fasta akaomba kufanya kikao kizito na mabosi wa klabu hiyo kinachofanyika leo Jumatatu kikiwa na ajenda nne kabla ya jioni kuibuka mazoezini kujitambulisha kwa wachezaji walioingia rasmi kambini tangu jana Jumapili.
Kikao hicho mbali na mabosi wa klabu, kitahusisha pia benchi nzima la ufundi ikiwa ni saa chache tangu kocha huyo awasili nchini tayari kuanza kazi ya kuinoa timu hiyo iliyomtambulisha Desemba 19 kuchukua nafasi ya Dimitar Pantev aliyesitishiwa mkataba mapema mwezi huu.
Habari kutoka ndani ya klabu ya Simba zinasema kuwa kikao hicho cha Barker msingi wake ni kupanga muelekeo mpya wa timu, baada ya kipindi kigumu ambacho kimepitia katika mashindano ya ndani na ya kimataifa.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, kikao hicho kitajadili kwa kina masuala manne makubwa yanayohusu hatima ya timu kwa sasa na siku za usoni.
“Kocha ametaka kukutana na benchi pamoja na viongozi kesho (leo) Jumatatu kujadili mambo manne kabla ya jioni kwenda kuonana na wachezaji na kuzungumza nayo, ikiwa ndio mwanzo wa Msauzi huyo kuanza rasmi kazi Msimbazi,” kilisema chanzo hicho cha kuaminika.
Ajenda hizo ni ushiriki wa Simba katika michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026 iliyoanza visiwani Zanzibar, timu hiyo ikipangwa Kundi B pamoja na Muembe Makumbi na Fufuni zote za visiwani humo pia tathmini ya kikosi na mipango ya usajili wa dirisha dogo linalofunguliwa Januari 1 mwakani.
Ajenda nyingine ni mwenendo wa timu katika michuano ya kimataifa ikiwa Kundi D katika Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na kufanya tathmini ya hali iliyonayo timu katika Ligi Kuu Bara na michuano ya Kombe la Shirikisho (FA) iliyoanza kwa raundi ya awali mapema mwezi huu.
Michuano ya Kombe la Mapinduzi imepewa uzito katika mipango ya kocha huyo raia wa Afrika Kusini, kwani itakuwa ni fursa ya kutazama kikosi hicho na kuingiza mbinu zake kabla ya majukumu mazito yaliyopo mbele yake. Barker anatarajiwa kuanza mazoezi na wachezaji waliokwisha ripoti kambini tangu jana kwa kuibuka jioni ya leo mara baada ya kikao hicho muhimu kwa mustakabali wa timu hiyo.
Hata hivyo, kikosi hicho hakitakuwa kamili kwani baadhi yao wapo katika majukumu ya kuzitumikia timu za taifa katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 inayoendelea Morocco.
Wachezaji waliopo AFCON na ambao huenda wakaungana na wenzake katika michuano ya Kombe la Mapinduzi ni pamoja na wale waliopo na Taifa Stars, Morice Abraham, Wilson Nangu, Kibu Denis, Yusuf Kagoma, Shomary Kapombe na Seleman Mwalimu, huku kipa Yakoub Suleiman aliyekuwa na timu hiyo akiwa ni majeruhi baada ya kuumia mazoezini kabla ya kuanza kwa michuano hiyo.
Pia Steve Mukwala anatumika na timu ya taifa ya Uganda iliyopo kundi moja na Tanzania, Tunisia na Nigeria. Hatma ya Yakoub kujiunga na kikosi itategemea ripoti ya madaktari wa klabu pamoja na hali yake ya kiafya, lakini kupitia Kombe la Mapinduzi, Barker anatajwa kuwa atafanya tathmini ya kina ya kikosi, hatua itakayomsaidia kufanya uamuzi mgumu lakini muhimu, ikiwamo kubariki au kupendekeza kuachana na baadhi ya wachezaji ambao hawataendana na falsafa yake ya soka.
Mashindano hayo yatamsaidia kubaini maeneo yenye upungufu ili kupendekeza maingizo mapya katika dirisha dogo la usajili, suala ambalo linatajwa kuwa sehemu ya mjadala mzito katika kikao cha leo.
Katika eneo la michuano ya kimataifa, Barker anakutana na kibarua kigumu cha kurejesha matumaini ya Simba yaliyoanza kufifia baada ya mwanzo mbaya katika makundi.
Simba ilianza kwa kupoteza mchezo wa kwanza nyumbani bao 1-0 dhidi ya Petro Luanda ya Angola, kabla ya kwenda kupoteza tena 2-1 kwa Stade Malieni ya Mali na kuiacha ikiburuza mkia kundini.
Matokeo hayo yaliwafanya mabosi wa klabu hiyo kufanya uamuzi mgumu wa mabadiliko ya kiufundi, ikiwamo kuachana na Dimitar Pantev.
Licha ya hali hiyo, Simba bado ina nafasi ya kupambana na kutinga hatua ya robo fainali iwapo itafanya vizuri katika mechi zilizobaki kama ilivyowahi kufanya msimu wa 2022-2023 wa michuano hiyo ilipopoteza mechi mbili za awali dhidi ya AC Horoya ya Guinea na Raja Casablanca, lakini ikazinduka ilipoumana na Vipers ya Uganda ikiifunga nje ndani kwa bai 1-0, kisha kuifumua Horoya mabao 7-0.
Simba imesaliwa na mechi nne muhimu ikiwamo mbili mfululizo dhidi ya Esperance ya Tunisia zitakazochezwa kati ya Januari 23 na 30 mwakani ikiwa ni kibarua cha kwanza kwa kocha Barker.
Baada ya hapo Simba itakamilisha makundi kwa kurudiana na Petro Luanda ugenini na kuisubiri Stade Malien kumalizana nao nyumbani zote zikipigwa mapema Februari mwakani.
Kwa upande wa Ligi Kuu Bara hali ya Simba sio mbaya sana japo ilipoteza mechi moja dhidi ya Azam iliyowanyoa mabao 2-0, baada ya awali kushinda mechi tatu mfululizo na kukusanya pointi tisa zilizoiacha nafsi ya tano hadi ligi hiyo iliposimama kupisha fainali za AFCON 2026.
Kwa ujumla, ujio wa Steve Barker umefungua ukurasa mpya ndani ya klabu ya Simba, huku macho na matumaini ya mashabiki yakielekezwa kwake kuona kama ataweza kurejesha uimara wa timu hiyo ndani ya nchi na katika michuano ya kimataifa.
Mashindano ya Kombe la Mapinduzi yanatajwa kuwa mwanzo wa safari hiyo mpya, safari ambayo ina matumaini lakini pia changamoto kubwa mbele yake.