
BAADA ya kurejea ndani ya kikosi cha Singida Black Stars, mshambuliaji Muivory Coast, Joseph Guede, ameanza na mguu mzuri kwa kufunga bao lililoihakikishia pointi tatu timu hiyo katika ushindi wa 3-1 dhidi ya Mlandege.
Guede ambaye aliitumikia Singida Black Stars msimu uliopita 2024-2025 alipotua dirisha kubwa akitokea Yanga, aliondoka kikosini hapo baada ya kucheza kwa takribani miezi mitano, akapewa thank you dirisha dogo.
Kurejea kwake, leo Desemba 28, 2025 amefunga bao katika mechi ya kwanza ya Kombe la Mapinduzi 2026 wakati Singida Black Stars ikiichapa Mlandege 3-1 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja.
Katika mechi hiyo ya ufunguzi kunako Kundi A, Guede alifunga bao hilo dakika ya 90 kwa ustadi mkubwa akimuinulia mpira kipa wa Mlandege, Hamadi Ubwa Baro aliyelala akijaribu kuwahi kuokoa hatari.
Kabla ya Guede kupachika bao hilo, Mlandege ilikuja juu ikipambana kusawazisha wakati matokeo yakiwa 2-1, lakini ikazimwa na bao hilo.
Idriss Diomande alianza kuifungia Singida Black Stars dakika ya 72 baada ya mabeki wa Mlandege kujichanganya wakati wakipambana kuokoa hatari.
Dakika ya 77, Emmanuel Keyekeh akaongeza bao la pili kwa Singida Black Stars akimalizia mpira uliitewa na Baro aliyekuwa akiokoa shuti la Elvia Rupia.
Said Khamid Matola maarufu Kunguru, akairudisha mchezoni Mlandege akifunga bao dakika ya 80, lakini Guede akaimaliza kabisa mechi kwa bao la dakika 90.
Kipindi cha kwanza ambacho kilikuwa na purukushani za hapa na pale, Mlandege ilijinyima nafasi ya kuongoza baada ya mwamuzi kuipa mkwaju wa penalti dakika ya 14 kufuatia Aimar Hafidh ‘Haaland’ kuangushwa eneo la hatari, lakini kiungo Yussuf Suleiman Haji ‘Jusa’ shuti lake likapanguliwa na Metacha Mnata.
Mlandege ambayo ni bingwa mtetezi, sasa ina cha kujiuliza mechi ijayo Desemba 31, 2025 itakapocheza dhidi ya URA ambapo siku hiyo pia Singida Black Stars itapambana na Azam.