TIMU ya Kagera Sugar imeweka rekodi mpya katika Ligi ya Championship msimu huu, baada ya kikosi hicho kinachonolewa na Juma Kaseja kushinda mechi tisa mfululizo, ikifuatiwa na Geita Gold na Mbeya Kwanza zilizoshinda mara nane kila mmoja.

Kagera iliyodumu katika Ligi Kuu Bara kwa miaka 20 tangu iliposhiriki 2005, ilishuka daraja msimu wa 2024-2025, baada ya kikosi hicho kushinda mechi tano, sare nane na kupoteza 17, ikishika nafasi ya 15, kufuatia kukusanya pointi 23.

Timu hiyo tangu ilipoanza ufunguzi wa Ligi ya Championship msimu huu kwa suluhu (0-0), dhidi ya maafande wa Transit Camp Oktoba 10, 2025, imeshinda mechi tisa mfululizo, ikiwa ni rekodi mpya kwa kikosi hicho kwani ilikuwa haijawahi kutokea.

Baada ya suluhu hiyo, Kagera ilizifunga Barberian mabao 2-1, (1-0) v Bigman FC, (4-1) v African Sports, (4-0) v Stand United, (2-0) v Polisi Tanzania, (1-0) v B19 FC, (3-1) v Hausung FC, (1-0) v TMA FC, kisha kuichapa Mbuni FC mabao 2-0.

Kabla ya kucheza jana, Jumapili kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba mkoani Kagera dhidi ya Songea United, timu hiyo tayari imecheza mechi 11, msimu huu, ambapo kati ya hizo imeshinda tisa na kutoka sare miwili, huku ikiwa haijapoteza yoyote.

Akizungumzia mwenendo wa timu hiyo, kocha wa kikosi hicho, Juma Kaseja, amesema siri kubwa ni kila mmoja kujitambua pia malengo waliyojiwekea mwanzo mwa msimu huu, huku ushirikiano wake mzuri na wachezaji ukiwa silaha nyingine inayowabeba.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *