WAANDAAJI wa mashindano ya Kombe la Mapinduzi 2026, wameitangaza Benki ya NMB kuwa mdhamini mkuu kwa kipindi cha miaka mitano, huku Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ikipongeza.
Hayo yamesemwa leo Desemba 28, 2025 mbele ya waandishi wa habari kisiwani Unguja ambapo SMZ, imeipongeza NMB kwa kusaini mkataba huo mnono wa zaidi ya Sh600 milioni kila mwaka.
Kwa kuingia udhamini huo, sasa mashindano yataitwa NMB Mapinduzi Cup 2026, huku msimu huu yakishirikisha timu 10 ambazo ni Yanga, Simba, Azam, Singida Black na TRA United za Tanzania Bar. Mlandege, KVZ, Fufuni FC na Muembe Makumbi City za Zanzibar, pamoja na URA ya Uganda inayoshiriki kama timu mwalikwa.
Akizungumza wakati wa hafla ya kusaini mkataba huo, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo wa SMZ, Riziki Pembe Juma, ameishukuru NMB kwa kuyapa hadhi na thamani mashindano hayo na kwamba imeonesha kwa vitendo inavyojali mashirikiano na Serikali yake.
Amebainisha kuwa, mkataba huo wa miaka mitano wa NMB, ni muendelezo wa ushirikiano uliotukuka baina ya benki hiyo na SMZ na kwamba wao kama Serikali wanaahidi kuyadumisha kwa maslahi mapana ya Wazanzibar na Watanzania kwa ujumla.
“NMB mmetuonesha uzalendo mkubwa, kwa kukubali kusaini mkataba huu na Kamati ya Mashindano kwa niaba ya Serikali. Tunaahidi kudumisha mashirikiano na benki hii, ambayo udhamini wao huu unaenda sio tu kubadili taswira ya mashindano, bali ndio mkubwa na mnono zaidi kuwahi kutolewa.
“Hata ukiangalia eneo la zawadi zao watakazokuwa wanatoa kwa Mchezaji Mwenye Nidhamu wa Mechi (Fair Play Awards) hatua ya makundi, nusu fainali na hadi fainali, zinaakisi dhamira yao ya kuyaboresha na kuyapa msisimiko mkubwa mashindano haya,” amesema Waziri Pembe.
Awali, Mkuu wa Idara ya Mauzo na Mtandao wa Matawi ya NMB, Donatus Richard, alisema wanajivunia ushirikiano wao wa miaka 13 ya mashindano hayo, na kwamba udhamini wao mkuu kwa kipindi cha miaka mitano, ni kielelzo cha juhudi za taasisi yake katika kuisapoti SMZ.
“Udhamini huu si tu kwaajili ya kufanikisha shughuili za NMB Mapinduzi Cup 2026, bali ni juhudi ya NMB kushirikiana na SMZ katika kuitangaza chapa ya visiwa vya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, na hii ndiyo maana halisi ya ushiriki wa sekta binafsi kwenye kuitangaza nchi kimataifa.
“Kama Mdhamini Mkuu wa NMB Mapinduzi Cup, tutashirikiana na Kamati ya Maandalizi katika maeneo makuu ya maandalizi na uendeshaji wa mashindano, ambapo baadhi ya tutakayofanya ni pamoja na kukabidhi zawadi kwa mshindi wa tuzo za Fair Play katika kila mchezo.
“Kwa hatua ya makundi, NMB itatoa tuzo hiyo sambamba na pesa taslimu Sh500,000 kwa Mchezaji Mwenye Nidhamu, kiasi ambacho kitaongezeka na kuwa Sh1 milioni kwenye hatua ya nusu fainali na Sh2 milioni kwenye mechi ya Fainali mbele ya Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi,” amebainisha Donatus.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya NMB Mapinduzi Cup 2026, Machano Makame Haji, aliishukuru Benki ya NMB kuyabeba mashindano hayo na kuyafanyia mapinduzi ya kimaboresho yanayoipa hadhi ya kimataifa michuano hiyo.
Mbele ya Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Ali Abdulghulam Hussein, Makame Haji alisema Kamati yake ilipokutana na NMB kujadili udhamini wa mashindano yao, haikuwachukua muda kukubaliana, na hivyo kuingia mkataba huo.
Naye Katibu wa Kamati ya Mashindano hayo, Rashid Said Suleiman, kwa upande wake alikiri kuvutiwa na unono wa mkataba wao na MB na kwamba makubaliano yao ya miaka mitano, ni hatua muhimu katika ukuaji, ustawi na maendeleo ya michezo Zanzibar.
“Mkataba huu (ambao yeye aliusaini kwa niaba ya Serikali), ni hatua muhimu mno katika ukuaji, ustawi na maendeleo ya mchezo, hususani mpira wa miguu hapa Zanzibar, kwani unaipa Kamati uhakika wa fedha kuimarika kwa mashindano,” amesisitiza Katibu huyo.