
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imevunja ukimya wake kuhusu hali ya mvutano unaoendelea nchini Somalia na Somaliland, na kuthibitisha uungaji mkono wake kwa Somalia.
Jumuiya ya Afrika Mashariki imesema kuwa, inaunga mkono kikamilifu nmamlaka ya nkujitawala Somalia kufuatia hatua ya Israel ya kulitambua rasmi eneo la ‘Somaliland, ambalo limejitenga na Somalia, kama taifa huru na lenye mamlaka kamili.
Taarifa ya sekretarieti ya jumuiya hiyo iliyotolewa Jumapili, Desemba 28, EAC ilisema inatambua Jamhuri ya Shirikisho la Somalia kuwa nchi moja huru chini ya mamlaka ya serikali ya Shirikisho la Jamhuri ya Somalia chini ya Rais Hassan Sheikh Mohamud.
Ijumaa iliyopita Somalia ilipinga vikali kile ilichoeleza kuwa ni hatua isiyo halali ya Israel kutambua eneo lake lililojitenga, Somaliland, kama taifa huru. Serikali ya Mogadishu imetaja uamuzi huo kuwa ni uvunjaji wa mamlaka na umoja wa ardhi ya taifa.
Somalia imeitaka Israel kubatilisha hatua yake ya kulitambua rasmi eneo la ‘Somaliland, ambalo limejitenga na Somalia, kama taifa huru na lenye mamlaka kamili. Somalia imelaani hatua hiyo na kuitaja kuwa kitendo cha “uchokozi ambacho kamwe hakitavumiliwa. Umoja wa Afrika (AU) pia umepinga vikali jaribio lolote la kutambua eneo lililojitenga la Somaliland kama taifa huru, ukisisitiza tena dhamira yake thabiti ya kulinda umoja, mamlaka na mipaka ya ardhi ya Somalia.
Somaliland ilijitenga na Somalia mwaka 1991 kufuatia vita vikali vya wenyewe kwa wenyewe lakini haijawahi kutambuliwa rasmi na nchi yoyote mwanachama wa Umoja wa Mataifa. Jamhuri hiyo iliyotangaza kujitenga na Somalia imeanzisha sarafu yake, bendera na bunge, ingawa maeneo yake ya mashariki yameathiriwa na mzozo.