
BAADA ya kurejea kuitumikia Singida Black Stars, mshambuliaji Muivory Coast, Joseph Guede ameonekana kupandisha mzuka kikosini hapo.
Guede ambaye amewahi kucheza Yanga kwa miezi sita msimu wa 2023-2024, kisha muda kama huo ndani ya Singida Black Stars msimu wa 2024-2025, amerejea kwa Walima Alizeti hao na atatambulishwa rasmi pindi usajili wa dirisha dogo utakapofunguliwa Januari Mosi 2026.
Mshambuliaji huyo ambaye kwa sasa yupo na Singida katika michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026 iliyoanza Desemba 28, 2025 kwenye Dimba la New Amaan Complex, Unguja, ameanza vizuri kwa kufunga bao moja katika ushindi wa 3-1 walioupata dhidi ya Mlandege.
Dakika 45 pekee zilimtosha mshambuliaji huyo kuanza maisha mengine ndani ya Singida akiingia mwanzoni mwa kipindi cha pili akichukua nafasi ya Deus Kaseke, kisha dakika ya 90, akafunga bao la kuhitimisha mechi.
Kocha Msaidizi wa Singida Black Stars, David Ouma, amezungumzia kurejea kwa Guede akisema uwepo wake utazidi kuimarisha safu yao ya ushambuliaji kwa kusaidiana na nyota wengine wa eneo hilo akiwamo Elvis Rupia, huku akiamini suala la kushindwa kufunga mabao mengi linakwenda kutatuliwa kikosini hapo.
“Umeona tumemleta Joseph Guede, amefunga bao zuri sana. Jambo zuri kuona kipindi hiki wachezaji wapya tuliowaleta wanaonyesha kitu kuelekea maandalizi ya mechi zijazo za kimataifa.
“Wachezaji wamekuwa na ubunifu mzuri sana, wanafuata maagizo kwa kuingia ndani ya boksi la mpinzani kwani huwezi kufunga mabao ya kutosha kama hujaingia katika boksi la mpinzani. Kufunga mabao matatu imetuonyesha tumeanza kurudi kivingine.
“Sasa hivi tumeamua kubadilika tofauti na tulivyozoeleka tukipiga pasi nyingi, tunaleta wachezaji wa eneo la mbele wenye uwezo wa kufunga.
“Tunatengeneza kitu ambacho tunataka wachezaji wetu wafunge mabao mengi, ukiangalia mechi tano za mwisho hatukuwa tunafunga mabao ya kutosha, hivyo tunajaribu kubadilisha hiyo kwanza tuwe wengi katika boksi la mpinzani iwe rahisi kufunga, kisha ndio tumiliki mpira,” amesema Ouma.