Waziri Mkuu wa Iraq amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haiingilii masuala ya ndani ya nchi hiyo ya Kiarabu.

Mohammed Shia’ al-Sudani ameeleza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haijaingilia au kuwa na ushawishi wowote katika masuala ya ndani ya Iraq, na kwamba uhusiano kati ya nchi hizo mbili umejengwa kwa kuzingatia mambo ya kidini na kitamaduni na uungaji mkono wa Tehran kwa Baghdad katika mapambano dhidi ya ugaidi.

Waziri Mkuu wa Iraq Mohammed Shia al-Sudani amesema hayo katika mahojiano maalum na Kanali ya Televisheni ya Al-Mayadeen na kufafanua kwamba katika miaka mitatu iliyopita ambayo ameshikilia wadhifa wa Waziri Mkuu, hakukushuhudiwa uingiliaji wa aina yoyote ile wa Iran katika masuala ya ndani ya Iraq.

Al-Sudani amesisitiza kwamba uhusiano kati ya Iran na Iraq ni mzuri na unaendelea katika ngazi rasmi, kisiasa, na kiraia.

Akizungumzia uungaji mkono wa Iran katika kukabiliana na Kundi la kigaidi la Daesh na kuunga mkono mchakato wa kisiasa wa nchi hiyo, Waziri Mkuu wa Iraq pia amesema kwamba kusimama kwa Iran pamoja na watu wa Iraq na serikali haimaanishi kutawala au kudhibiti maamuzi; badala yake, kunamaanisha ushirikiano katika kalibu ya ujirani.

Al-Sudani pia amekumbushia pia msimamo thabiti wa Iraq kuhusu suala la Palestina, akilaani uvamizi dhidi ya Ukanda wa Gaza na Lebanon, na matukio nchini Syria, na akasema kwamba dira ya sera ya Iraq daima imekuwa ni maslahi ya kitaifa ya nchi hiyo, na haitasalimu amri kwa mashinikizo kutoka upande wowote ule.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *