WINGA wa zamani wa Simba, Rashid Juma Mtabigwa, ameonekana akiichezea Mlandege katika michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026 inayoendelea kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja, huku kocha msaidizi wa kikosi hicho, Sabri Ramadhan ‘China’ akitoa ufafanuzi wa uwepo wa nyota huyo mchachari.

Katika mechi hiyo ambayo Mlandege ilifungwa 3-1 na Singida Black Stars ikichezwa Desemba 28, 2025, Mtabigwa aliingia dakika ya 67 kuchukua nafasi ya Yussuf Suleiman Haji ‘Jusa’.

Nyota huyo mbali na kutmba na Simba, lakini amewahi kuzitumikia Polisi Tanzania, Ruvu Shooting, Ihefu (sasa Singida Black Stars), Mtibwa Sugar na TMA Stars ya Championship kabla ya sasa kuibukia Mlandege inayotetea taji.

Akizungumzia ujio wa winga huyo ndani ya Mlandege, China amesema: “Ndio yupo, lakini hayo ni maongezi ya uongozi na mchezaji, mimi siwezi kusema mengi zaidi kwa sababu leo (juzi) nimeletewa nimuone.

“Kwa muda aliocheza nimemuona ni mchezaji mzuri sana, kwa sababu anajiamini, lakini spidi imepungua nadhani kwa sababu ya uchovu wa safari.”

Winga huyo akiwa ameibukia Mlandege, Septemba 19, 2025 alitambulishwa kuwa mchezaji wa TMA Stars inayoshiriki Ligi ya Championship Tanzania Bara ambayo juzi ilichapwa 2-1 na Polisi Tanzania, siku ambayo pia Mlandege ilikula 3-1 kutoka kwa Singida.

Mbali na Simba ambapo msimu wa 2017-2018 alitangazwa kuwa mchezaji chipukizi klabuni hapo, winga huyo amecheza Polisi Tanzania, Ruvu Shooting, Mtibwa Sugar na Ihefu ambayo baadaye ilipobadilishwa kuwa Singida Black Stars akaendelea kuwepo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *