Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Badr Abdelatty, Jumatatu alitoa wito wa kufanyika kikao cha dharura cha Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika ili kupinga hatua ya utawala wa Israel kutambua jimbo lililojitenga na Somalia la Somaliland kama nchi huru.

Akizungumza katika mkutano wa mawaziri kwa njia ya mtandao, Abdelatty alieleza kuwa hatua ya Israel ni “ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa, Mkataba wa Umoja wa Mataifa na Hati ya Umoja wa Afrika.”

Ameonya kuwa utambuzi huo unadhoofisha misingi ya amani na usalama wa kikanda na kimataifa, hususan katika eneo la Pembe ya Afrika. Abdelatty amesisitiza haja ya kikao cha dharura cha AU ili kujadili suala hilo na kulinda umoja na mipaka ya Somalia, sambamba na kukataa hatua zinazotishia amani na usalama wa kikanda na kimataifa.

Jumapili, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ilitoa wito kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuchukua msimamo thabiti dhidi ya utambuzi wa Israel kwa Somaliland. Katika taarifa baada ya kikao cha dharura mjini Cairo, jumuiya hiyo ilisisitiza haki ya Mogadishu kujilinda na kutetea ardhi yake.

Ukosoaji wa kimataifa umeongezeka dhidi ya hatua ya Israel, mataifa mengi yakieleza kuwa ni ukiukaji wa sheria za kimataifa na tishio kwa uthabiti wa kikanda.

Ijumaa, Somalia ilirejelea msimamo wake thabiti na usioweza kujadiliwa kuhusu uhuru wake, umoja wa kitaifa na mipaka yake, kufuatia kitendo cha kichokozi cha Israel kutambua jimbo la Somaliland kama nchi huru.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *