HEBU fikiria. Wewe ni mchezaji, inatoka listi ya wanaoanza kikosi cha kwanza katika mechi, jina lako lipo, lakini baada ya dakika 28 tangu kipute kuanza, unaitwa benchi. Nafasi yako anachukua mwingine. Bila shaka utakuwa na maswali mengi yasiyokuwa na majibu.
Achana na hilo. Kuna ile listi inatoka, jina lake unajiona unaanzia benchi, kiroho safi unajiandaa kisaikolojia lolote linaweza kutokea na ukapata nafasi ya kuingia.
Muda wako unafika unapewa nafasi, lakini dakika 23 tu zinaonekana zimekutosha kutoa mchango wako. Unaitwa urudi benchi.
Sasa basi, hayo yamewakuta nyota wawili wa TRA United, Ramadhan Chobwedo na Adam Omar Adam wakati kikosi hicho kikipambana na KVZ katika mechi ya Kombe la Mapinduzi 2026.
Mechi hiyo iliyochezwa Desemba 29, 2025, kwenye Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Unguja, ilimalizika kwa sare ya bao 1-1. TRA United ilianza kufunga dakika ya 54 kupitia Enock Mkanga aliyeunganisha kwa kichwa kona iliyopigwa na Abdulhamid Ramadhan, kisha KVZ ikasawazisha dakika ya 66, mfungaji akiwa Michael Joseph Godlove.
ILIVYOKUWA
Dakika ya 28, Ndayiragije alimuinua Abdulhamid Ramadhan ambaye alienda kuchukua nafasi ya Chobwedo aliyeonekana kama ameshindwa kufanya kile alichoagizwa.
Mabadiliko hayo yalizaa matunda kwani bao la TRA United lilifungwa kutokana na kona iliyopigwa na nyota huyo aliyetokea benchi.
Muda mchache baada ya TRA kuongoza, Ndayiragije akaona anahitaji mabao zaidi, dakika ya 57, anafanya mabadiliko kwa kumtoa James Msuva, anaingia Adam.
Bila ya kutarajia, dakika ya 80, zikiwa zimepita takribani dakika 23 tangu aingie, anarudishwa benchi, anaingia Shaban Idd Chilunda.
Mabadiliko ya nyota hao, yalionekana kuwachukiza wachezaji wenyewe kwani walivyokuwa wanatoka, walionyesha sura za kutokuwa na furaha huku Adam akiwa anazungumza mwenyewe hadi anakwenda benchi.
Baada ya mechi hiyo, Ndayiragije alifafanua kwa kusema: “Katika mechi hakuna muda maalum wa kufanya mabadiliko, mwalimu huwa anaangalia mipango yake inakwendaje katika kile anachokitafuta.
“Ukiangalia katika mechi hii tumechezesha wacheaji takribani sita wapya, hivyo nilitaka kuwaona ndio maana nikawa natoa nafasi kama ulivyoona.” Sare hiyo sasa inailazimu TRA kuifunga Yanga katika mechi inayofuatia Januari 6, 2026 ili ifuzu hatua ya nusu fainali kwani kundi lao lenye timu tatu, inapenya moja yenye pointi nyingi. Kabla ya hapo, KVZ itacheza na Yanga Januari 4, 2026, mechi zikipigwa Uwanja wa New Amaan Complex kuanzia makundi hadi nusu fainali, kisha fainali itachezwa Januari 13, 2026 kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba.