Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu amesema kuwa, vitisho vya Trump dhidi ya Iran ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa.

Sayyid Abbas Araqchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amewaandikia barua mawaziri wenzake wa mambo ya nje wa nchi jirani na kutaka kulaaniwa waziwazi na kwa uthabiti; bwabwaja na upayukaji wa Trump na Netanyahu akitangaza kwamba, Iran haitosita kutoa jibu kali na la kumjutisha yeyote atakayeshiriki kwenye uchokozi dhidi yake.

Katika barua yake hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araqchi amesema kuwa, vitisho vya rais wa Marekani, Donald Trump dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa, na amemtaka kila mtu kulaani kwa uwazi na kwa uthabiti kauli hizo za kichochezi.

Jumatatu usiku, Disemba 29, na katika mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni, Donald Trump alitoa bwabwaja mpya alizozitia chumvi akisema: “Ikiwa Iran itaendelea na mpango wake wa makombora, nitaunga mkono kushambuliwa Iran. Ikiwa wataendelea na mpango wao wa nyuklia, tutashambulia mara moja.”

Katika barua yake hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amezungumzia upayukaji huo wa Trump na kusema: Tishio la kutumia nguvu dhidi ya Iran ni ukiukaji wa wazi wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa, ambao unakataza kutoa vitisho au matumizi yoyote ya nguvu dhidi ya nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa na kuhatarisha uhuru wa kitaifa wa nchi nyingine.

Akikumbushia mashambulio ya pamoja ya kijeshi na Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran yaliyoanza mwezi Juni 2025, Araqchi amesisitiza kwamba, vitisho hivyo vinaonesha nia mbaya na ya wazi ya Marekani na kwamba lawama za uchokozi wowote ule zitabebwa na yeye mwenyewe Trump.

Donald Trump

Waziri wa Mambo ya Nje, sambamba na kuonya kuhusu matokeo hatari ya kukaa kimya mbele ya vitisho hivyo na vitendo haramu, alisisitiza kwamba, kuunda mazingira ya kinga ya kutoshtakiwa kumezipa kiburi zaidi Marekani na utawala wa Israel cha kuendelea na tabia yao ya uchokozi na ni tishio la moja kwa moja dhidi ya amani na usalama wa dunia. Araqchi alimalizia kwa kusisitiza haki ya asili na isiyopingika ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kujilinda kwa mujibu wa kifungu cha 51 cha Mkataba wa Umoja wa Mataifa, na akasema kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitasita kutoa jibu kali kwa uchokozi wowote na kumfanya adui ajute.

Vitisho vya hivi karibuni vya Donald Trump dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vinaweza kutathminiwa kama ukiukaji wa wazi na mkubwa kwa mtazamo wa sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa. Mkataba wa Umoja wa Mataifa, ambao uliandikwa baada ya Vita vya Pili vya Dunia kama nguzo kuu ya utaratibu wa kimataifa, unakataza waziwazi tishio au matumizi yoyote ya nguvu dhidi ya umoja wa ardhi na mamlaka ya kisiasa ya mataifa.

Vitisho vya Trump vya kushambulia kijeshi Iran ikiwa itaendelea na mipango yake ya makombora au miradi ya nyuklia ni mfano wazi wa tishio. Kauli kama hizo hazihalalishiki katika kalibu ya kujilinda, wala Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halijatoa kibali cha kuchukua hatua za kijeshi. Kujilinda kunaruhusiwa tu chini ya kifungu cha 51 cha mkataba wa Umoja wa Mataifa wakati nchi iko chini ya shambulio la silaha. Hii ni katika hali ambayo, hakuna shambulio lolote lililofanywa na Iran dhidi ya Marekani, kwa hivyo kutumia hoja ya kujilinda hakuna msingi wowote.

Fauka ya hayo, vitisho vya Trump vinafanyika katika mchakato usio wa kisheria na wa kivamizi na mfano wa hilo, ulishuhudiwa Juni mwaka huu katika mashambulizi ya pamoja ya Marekani na Israel dhidi ya Iran. Mashambulizi haya yalifanywa kwenye miundombinu muhimu na vituo vya nyuklia vya amani nchini Iran na yalikuwa ukiukaji dhahiri wa sheria za kimataifa na kanuni za kibinadamu. Kukiri rasmi kwa Rais wa Marekani kuhusika moja kwa moja nchi yake katika mashambulizi hayo pia kunaibua suala la kufuatiliwa kisheria maafisa wa Marekani.

Kwa mtazamo wa sheria za kimataifa, vitisho vya Trump havihatarishi tu usalama wa Iran bali usalama wa eneo na dunia kwa ujumla. Mkataba wa Umoja wa Mataifa unasisitiza udumishaji wa amani na usalama wa kimataifa, na hatua yoyote au tishio linalozidisha mvutano ni kinyume na madhumuni ya taasisi hiyo. Vitisho hivyo vinaweza kusababisha mwelekeo hatari katika mahusiano ya kimataifa ambapo mataifa makubwa, bila kujali sheria na kanuni za kimataifa, hutumia nguvu au mabavu ili kusukuma magurudumu ya malengo yao ya kisiasa.

Radiamali ya Iran na akthari ya wanasheria wa kimataifa pia unategemea msingi huu. Katika barua kwa Baraza la Usalama na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, maafisa wa Iran wameona vitisho hivi kuwa ni ukiukaji mkubwa wa hati ya Umoja wa Mataifa na wametaka kulaaniwa hilo waziwazi. Wataalamu wa sheria za kimataifa pia wamesisitiza kwamba, hakuna sababu yoyote iliyotolewa na Marekani, ikiwa ni pamoja na madai ya kujilinda inayokubalika ndani ya mfumo wa sheria za kimataifa na vitendo kama hivyo havina uhalali wa kisheria.

Kwa muktadha huo inapasa kusema kwamba, vitisho vya Trump dhidi ya Iran ni mfano wazi wa sera ya upande mmoja na upuuzaji wa sheria za kimataifa. Vitisho hivi si tu kwamba ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa, lakini pia vinatilia shaka uaminifu na ufanisi wa mfumo wa kimataifa. Ikiwa jamii ya kimataifa haitatoa radiamali mwafaka kwa tabia hii, basi hatari ya kudhoofisha kanuni za msingi za sheria za kimataifa na kueneza ukosefu wa utulivu katika mahusiano ya kimataifa itaongezeka siku baada ya siku.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *