Ukatili wa kingono dhidi ya watoto limekuwa jambo la kawaida, la kimfumo na unazidi kuongezeka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Hii ni kwa mujibi wa ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF).

Takwimu za nchi nzima zilizokusanywa na watoa huduma za ulinzi na jinsia zinaonyesha kuwa, katika miezi tisa ya kwanza ya mwaka jana wa 2025, kulikuwa na zaidi ya kesi 35,000 za ukatili wa kingono dhidi ya watoto nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Mwaka juzi wa 2024, watoto walikuwa wahanga wa karibu asilimia 40 ya matukio yote yaliyoripotiwa ya vitendo vya ukatili wa kingono; kiwango  ambacho ni karibu mara tatu ya takwimu za mwaka 202o. 

Migogoro ndio chanzo kikuu cha ukatili huu tajwa hata hivyo shirika la UNICEF limeripoti uwepo wa ukatili wa kingono dhidi ya watotokatika kila jimbo huko Kongo.

UNICEF inafanya kazi na serikali ya Kongo na washirika wengine kutoa huduma ya matibabu kwa watoto, ushauri nasaha na msaada wa  kisaikolojia pamoja na kushughulikia kesi. 

Mwaka 2024 Unicef ilieleza kuwa imewafikia watoto zaidi ya 24,000 katika majimbo ya Kongo yaliyoathiriwa pakubwa na janga hilo.

Shirika la UNICEF limesema kuwa kupunguzwa ufadhili wa fedha kimataifa kunawaweka mamia ya maelfu ya watoto katika hatari, ikiwa ni pamoja na katika maeneo yaliyoathiriwa na vita mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *