Zohran Mamdani leo amekuwa Meya wa kwanza wa Jiji kubwa zaidi la Marekani la New York kuapishwa kwa kutumia Kitabu kitakatifu cha Qur’ani ya Msahafu mkongwe na wa kihistoria wa tangu karne mbili zilizopita.
Mamdani, ambaye ni Meya wa kwanza Muislamu wa Jiji la New York mwenye asili ya Asia Kusini na aliyezaliwa barani Afrika ametumia Msahafu wa babu yake wa tangu miaka 200 iliyopita ulioazimwa kutoka Maktaba ya Umma ya New York (NYPL) kwa ajili ya hafla ya faragha ya kuapishwa iliyofanyika katika kituo cha treni ya chini ya ardhi kilichokuwa hakitumiki chini ya eneo la Times Square.
Meya huyo mpya wa New York anapanga kutumia nakala mbili za Qur’ani ambazo zilikuwa za babu yake na bibi yake katika sherehe ya hadhara ya kula kiapo itakayofanyika kesho Ijumaa kwenye Ukumbi wa Jiji la New York.
Msahafu wa kihistoria alioshika kulia kiapo Mamdani ulioazimwa kutoka maktaba ya umma ya New York, uliwahi kuwa milki ya Arturo Alfonso Schomburg, mwanahistoria na mwandishi Mweusi ambaye aliuza majimui ya vitabu vyake 4,000 kwa NYPL mnamo mwaka 1926, ambavyo baadaye vilitumiwa kuasisi Kituo cha Utafiti wa Utamaduni wa Watu Weusi cha Schomburg.
Schomburg alizaliwa Puerto Rico katika miaka ya 1870 na wazazi wenye asili ya Ujerumani na Wacaribbean wenye asili ya Afrika…/
