
Mmoja wa viongozi waandamizi wa harakati ya ukombozi wa Palestina ya Fat’h amesema kuwa, Makubaliano ya Abraham ni udanganyifu wa kisiasa na hayatoleta utulivu katika eneo hili maadamu yanapuuza kadhia ya Palestina.
Katika maadhimisho ya miaka 61 ya kuanzishwa harakati ya Fat’h, Qadura Fares, mmoja wa viongozi wa harakati hiyo amesema kwamba, Fat’h itaendelea kudumu katika utekelezaji wa jukumu lake la uongozi katika mapambano ya kitaifa ya Wapalestina.
Amesema hayo kwenye mahojiano na tovuti ya habari ya televisheni ya Al-Alam na kusema: Mapambano ya wananchi wa Palestina yataendelea hadi wavamizi Wazayuni watakapotimuliwa kutoka kwenye ardhi ya Palestina.
Fares amezungumzia pia malengo ya njama za Kizayuni huko Palestina na kubainisha kuwa: Malengo ya utawala huo dhalimu ni kuwahamisha Wapalestina kwenye ardhi zao na ni kufanya mauaji ya umati na kuwapora Wapalestina ardhi zao ili jina la Palestina lifutike kwenye ramani ya dunia na kwenye jiografia ya kisiasa ulimwenguni.
Akibainisha kwamba Intifada ya kwanza ya Palestina ilikuwa hatua muhimu katika mapambano ya kitaifa ya Palestina, amesema: Mafanikio ya mapambano ya ukombozi wa Palestina yanatokana na ushawishi wa fikra ya kimapinduzi katika jamii ya Palestina na imefikia hatua ambayo kila Mpalestina anajikuta ni kama askari wa mstari wa mbele ya kupambana na Wazayuni wavamizi.
Kiongozi huyo mwandamizi wa harakati ya Fat’h ya Palestina ameongeza kuwa, makubaliano ya Oslo yalizusha mzozo wa ndani katika harakati hiyo.
Amesisitiza kwamba Intifada ya Al-Aqsa pia ilikuwa harakati maarufu, na Fat’h ilijaribu tangu mwanzo kuthibitisha kwamba ilikuwa mwaminifu kwa ahadi yake kwa mashahidi wa Palestina na ndio maana iliiunga mkono Intifadha hiyo.