
Msururu wa mapendekezo yaliyo mbele ya Bunge la Israel au Knesset, ya kupunguza vigezo vya matumizi ya adhabu ya kifo yanaibua wasiwasi mkubwa kuhusu ubaguzi dhidi ya wapalestina na ukiukwaji wa haki zao za kupata mchakato wa haki wa kisheria, pamoja na ukiukaji mwingine wa sheria za kimataifa za haki za binadamu na sheria za kibinadamu za kimataifa.
“Linapokuja suala la adhabu ya kifo, Umoja wa Mataifa uko wazi kabisa, na unaipinga chini ya mazingira yote. Ni vigumu sana kupatanisha adhabu hiyo na heshima ya binadamu, na inaleta hatari isiyokubalika ya kuwanyonga watu wasio na hatia.” ameeleza Türk.
Türk amesema mapendekezo haya hayalingani na wajibu wa Israel chini ya mkataba wa kimataifa wa haki za kiraia na kisiasa. Hasa, kuanzishwa kwa adhabu ya kifo ya lazima, ambayo haiachi mamlaka yoyote kwa mahakama, ni ukiukaji wa haki ya kuishi.
“Pendekezo hilo pia linaibua wasiwasi mwingine wa haki za binadamu, ikiwemo kwa misingi kwamba ni la kibaguzi kwani litatumika kwa Wapalestina pekee.” Ameongeza
Amesema lugha ya sheria hiyo inayopendekezwa, pamoja na kauli za wanasiasa wa Israel, zinaonesha kuwa inalenga kutumika kwa wapalestina pekee, ambao mara nyingi hukutwa na hatia baada ya kesi zisizo za haki.
Nini kitafanyika chini ya mapendekezo hayo
Mabadiliko yanayopendekezwa yangerekebisha sheria ya kijeshi inayotumika katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na Israeli, na kuyataka mahakama za kijeshi kutoa adhabu ya kifo ya lazima kwa hukumu zote za mauaji ya kukusudia katika eneo hilo.
Zaidi ya hayo, sheria hiyo ingerekebisha sheria ya adhabu ya Israel na kuanzisha adhabu ya kifo kwa mauaji ya kukusudia ya waisraeli katika vitendo vinavyoelezwa kuwa vya kigaidi. Sheria hiyo pia ingesababisha adhabu ya kifo kutumika kwa njia ya kurudi nyuma kwa waliopatikana na hatia ya mauaji yanayohusiana na mashambulizi ya kutisha ya tarehe 7 Oktoba 2023, jambo linalokiuka kanuni ya uhalali iliyoainishwa katika sheria za kimataifa.
Aidha, mabadiliko yanayopendekezwa kuhusu matumizi ya adhabu ya kifo yanajumuisha masharti yanayohusu vitendo vya “ugaidi, ubaguzi wa rangi au uhasama dhidi ya umma”, ambavyo vimefafanuliwa kwa njia isiyo wazi na pana kupita kiasi.
Mapendekezo hayo pia yanakiuka kanuni za sheria za kibinadamu za kimataifa zinazohusiana na taratibu za adhabu na utekelezaji wa adhabu ya kifo dhidi ya wakazi wa eneo linalokaliwa, ameongeza kamishna mkuu. Amekumbusha kuwa kumnyima Palestina yeyote kutoka ukingo wa magharibi na Gaza dhamana za kesi ya haki zilizobainishwa katika mkataba wa nne wa Geneva ni kosa la kivita.