Nchini Sudan, mapigano makali yamekuwa yakiendelea kwa siku kadhaa kati ya jeshi la serikali na wanamgambo wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) katika majimbo matatu ya Kordofan: Kordofan Kaskazini, Kordofan Kusini, na Kordofan Magharibi. Jeshi lilianzisha mashambulizi yake makubwa zaidi katika miezi mitatu katika eneo hili la kusini. Linadai kurejesha miji ya kimkakati iliyokuwa imeangukia mikononi mwa RSF, ambayo  inakataa kurudi nyuma.

Imechapishwa:

Dakika 2 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Nchini Sudan, jeshi linatafuta kurejesha mpango huko Kordofan, eneo ambalo RSF inatawala na/au kuzingira miji muhimu zaidi. Linadai kuwa linatoa shinikizo mara mbili kwenye mistari ya usambazaji ya chakula na risasi ya RSF kwenda Kordofan Kaskazini na linadai kuwa limerejesha miji kadhaa, na kulazimisha RSF kurudi nyuma kuelekea magharibi. Jeshi hilo limeongeza kuwa limeweza kupeleka vifaa kwa mji wa Dilling, ambao ulikuwa umezingirwa na RSF, huko Kordofan Kusini. Pia limeteka tena Hamadi, Habila, na Kazkil katika eneo hilo, miji iliyoko kusini mwa El-Obeid, mji mkuu wa Kordofan Kaskazini.

Vikosi vya pamoja vinavyoshirikiana na jeshi, kwa upande wao, vimetangaza kwamba vimechukua miji mingine huko Kordofan Kusini, kama vile Dbeibat, na kulazimisha RSF kujiondoa.

Hata hivyo, wanamgambo wa RSF wamekanusha waziwazi madai ya kuwa wamedhoofika huko Kordofan Kusini.

Kifo cha mshauri wa Jenerali Hemedti huko Darfur

Jeshi pia limetoa video za wanachama wa RSF waliokamatwa katika siku za hivi karibuni, wakiwemo mamluki wa Sudan Kusini. Khartoum kwa sasa inawasiliana na Sudan Kusini ili kuipa Juba ushahidi rasmi wa kuhusika huku kwa mamluki.

Hata hivyo, mshauri wa usalama wa Jenerali Hemedti huko Darfur aliuawa katika shambulio la anga la jeshi. Ni Mohamad Ali Abu Bakr, mshirika wa karibu wa Abderrahim Dogolo, kaka yake Hemedti. Alifariki wakati wa mkutano katikati mwa Darfur, karibu na Zalingei. Wenzake watano pia waliuawa. Kifo chake kimethibitishwa na afisa wa RSF ambaye aliapa kulipiza kisasi. Kiongozi huyo wa mapambano aliongoza kikosi cha mamia ya wapiganaji wanaojulikana kama al-Saif al-Battar, ikimaanisha “upanga mkali.” Alikuwa na jukumu kubwa katika kuajiri makabila kupigana pamoja na RSF.

Vita nchini Sudan, ambavyo ni kati ya jeshi la Jenerali al-Burhan na wanamgambo wa Jenerali Hemedti tangu mwezi Aprili 2023, vimegharimu maish ya makumi ya maelfu ya watu, na kusababisha watu milioni 11 kuyahama makzi yao, na kusababisha kile ambacho Umoja wa Mataifa unakiita “mgogoro mbaya zaidi wa kibinadamu duniani.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *