
Maelfu ya watu kutoka Iran na kote ulimwenguni wamekusanyika katika mji wa Kerman ulioko kusini mwa Iran, kuadhimisha kumbukizi ya kuuawa shahidi Luteni Jenerali Qassem, aliyekuwa kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC.
Waombolezaji wameadhimisha kumbukumbu ya mwaka wa 6 tangu kuuawa shahidi Jenerali Soleimani, ambaye alikuwa shujaa wa kupambana na ugaidi katika eneo la Asia Magharibi.
Mbali na mji huo wa Kerman alikozikwa Shahidi Soleimani, hauli ya kumkumbuka na kumuenzi shujaa huyo wa Muqawama imefanyika katika miji karibu yote ya Iran, kwa kuhudhuriwa na shakhsia mbalimbali wa kisiasa na kijamii, Maulamaa na baadhi ya wawakilishi wa mataifa mbalimbali duniani.
Marasimu ya kuadhimisha kumbukumbu ya kuuawa shahidi kwa kamanda huyo wa Muqawama yamefanyika katika Ukumbi wa Mosalla mjini Tehran, yakihudhuriwa na watu mashuhuri wa kisiasa, kitamaduni, kijeshi, na kijamii, pamoja na idadi kubwa ya wapenzi wa Luteni Jenerali Qassem Soleimani.
Jana Alkhamisi katika marasimu hayo kwenye Mosalla wa mjini Tehran, Rais Masoud Pezeshkian aliisisitiza kwamba, taifa la Iran litaendeleza njia ya Shahid Luteni Jenerali Qassem Soleimani na viongozi wengine wa kambi ya Muqawama akiongeza kuwa, shahidi Soleimani alikuwa nembo ya maelewano, huruma na utiifu kwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Luteni Jenerali Qassem Soleimani aliuawa shahidi Januari 3, 2020 katika shambulio la anga lililofanywa na jeshi vamizi na la kigaidi la Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad, akiwa pamoja na Abu Mahdi al Muhandis, aliyekuwa Naibu Mkuu wa harakati ya kujitolea ya wananchi wa Iraq ya al Hashd al Sha’abi na wanamapambano wengine wanane, wakati alipoelekea Iraq kwa mwaliko rasmi wa serikali ya nchi hiyo.