Tehran imeonya kuhusu matokeo mabaya ya vitisho vya hivi karibuni vya Marekani dhidi ya mpango wa nyuklia wa amani wa Iran.
Ikijibu vitisho vya hivi karibuni vya Marekani dhidi ya mpango wa nyuklia wa amani wa Iran, Ofisi ya Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Mashirika ya Kimataifa huko Vienna imemtumia barua Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), ikionya kuhusu matokeo hatari ya kuendelezwa vitisho hivyo kwa hadhi ya shirika hilo na mfumo wa kimataifa wa kuzuia kuenezwa silaha za nyuklia.
Ujumbe wa ofisi hiyo uliotolewa kwenye mtandao wa kijamii wa X Jumatano wiki hii, umeonya kwamba: Kukaririwa vitisho hivyo kunahatarisha hadhi ya Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki na kudhoofisha hali ya kuaminiana kimataifa. Ujumbe huo unaongeza kuwa: Vitendo hivyo vya kijinga lazima vilaaniwe, na wahusika wawajibishwe kikamilifu.
Ujumbe huo unakuja huku Rais wa Marekani, Donald Trump akikariri maneno na vitisho vya zamani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran siku ya Jumatatu, Disemba 29, baada ya kukutana na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu. Trump alitoa madai dhidi ya Iran akisema: “Nimesikia kwamba Iran inajaribu kujenga upya (uwezo wake wa nyuklia) na ikiwa itafanya hivyo, tutauharibu. Natumai hilo halitatokea.”
Alipoulizwa kama anamruhusu Netanyahu kuishambulia tena Iran, Trump alisema: “Kwa ajili ya makombora ya balestiki, ndiyo. Kwa ajili ya silaha za nyuklia, haraka sana!”

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Sayyid Abbas Araqchi amevitaja vitisho vya Rais wa Marekani kuwa ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa na hati ya Umoja wa Mataifa, na ametoa wito wa kulaaniwa vikali matamshi hayo ya kichochezi. Akisisitiza haki isiyopingika ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kujilinda kwa mujibu wa Kifungu cha 51 cha Hati ya Umoja wa Mataifa, Araqchi amesema kwamba, Jamhuri ya Kiislamu haitasita kutoa jibu kali na kujutisha kwa uchokozi wowote.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia, imetuma barua mbili tofauti kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Rais wa Baraza la Usalama la umoja huo ikipinga viikali matamshi ya kichochezi na vitisho vya Rais wa Marekani.
Inaonekana kuwa vitisho vya mara kwa mara vya Marekani dhidi ya mpango wa nyuklia wenye malengo ya amani wa Iran ni zaidi ya mzozo wa kisiasa au kiusalama wa pande mbili, na vina athari kubwa kwa hadhi na itibarii ya taasisi za kimataifa na mfumo wa kimataifa wa kuzuia kuenea kwa silaha za nyuklia. Mbali na kudhoofisha hali ya kuaminiana kati ya nchi mbalimbali, vitisho hivyo pia vinaunda polepole mwenendo hatari wa kuhalalisha mashinikizo ya kisiasa dhidi ya shughuli halali na za kisheria za nyuklia. Mwelekeo kama huo unaweza kudhoofisha misingi ya kisheria na kimaadili ya mfumo wa kimataifa.
Mpango wa nyuklia wa Iran unatekelezwa chini ya Mkataba wa Kutoeneza Silaha za Nyuklia (NPT) na chini ya usimamizi wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA). Iran imetangaza mara kwa mara kwamba lengo lake ni kutumia nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani na katika maeneo kama vile uzalishaji wa umeme, dawa na kilimo. Hata hivyo, vitisho vya Marekani na baadhi ya washirika wake vinatambulisha shughuli hizo kama hatari tarajiwa; na kwa kutumia zana za kisiasa na kiuchumi, vinajaribu kubana njia ya Iran ya kuelekea kwenye ustawi wa kisayansi na kiteknolojia. Mbinu hii inatoa changamoto kwa kanuni ya msingi ya haki ya mataifa mbalimbali kutumia nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani.
Inatupasa kusema kuwa, kuendelea kwa vitisho vya Marekani dhidi ya mpango wa nyuklia wa amani wa Iran kutakuwa na matokeo mabaya.
Matokeo ya kwanza ya vitisho hivyo ni kudhoofika hadhi na itibari ya Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA). Shirika hilo ni taasisi ya kiufundi na maalumu iliyopewa jukumu la kutathmini shughuli za nyuklia za nchi mbalimbali kwa mujibu wa vigezo vya kisayansi na kisheria. Kwa sababu, wakati maamuzi na ripoti za shirika hilo zinapokabiliwa na mashinikizo ya kisiasa kutoka kwa mataifa makubwa, imani ya kimataifa kuhusu kutokuwa na upendeleo na uhuru wa taasisi hiyo hupungua sana.
Inasikitisha kwamba, jibu lisilo na msingi la Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki, kwa shambulio la Marekani na Israel dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran wakati wa vita vya siku 12 limezidisha kiburi cha Trump na kumpa fursa ya kutoa vitisho vya hivi karibuni dhidi ya mpango wa nyuklia wa amani wa Iran.

Matokeo mabaya ya pili ya vitisho hivyo ni kutoa pigo kwa mfumo wa kimataifa wa kutosambaza silaha za nyuklia, ambao unategemea kuheshimiwa majukumu ya pande zote husika. Nchi zote zinajiepusha kumiliki silaha za nyuklia, na mkabala wake, zinadhaminiwa haki ya kutumia teknolojia ya nyuklia kwa malengo ya amani. Vitisho vya Marekani dhidi ya Iran vinavuruga mlingano huo.
Matokeo ya tatu ni kuhalalisha matumizi ya vitisho kama zana na wenzo wa sera ya kigeni. Wakati vitisho dhidi ya shughuli halali katika nchi moja mwanachama wa Umoja wa Mataifa vinapokuwa jambo la kawaida, desturi hii inaweza kupanuliwa na kutumiwa katika maeneo mengine. Kwa sababu katika siku zijazo, nchi mbalimbali zenye nguvu ya kijeshi zinaweza kutumia vitisho na mashinikizo ili kuzuia mafanikio ya kisayansi au kiuchumi ya washindani wao. Mwelekeo kama huo sio tu kwamba unahatarisha usalama wa kimataifa, lakini pia unatia sumu mazingira ya ushirikiano wa kisayansi na kiteknolojia duniani.