
Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, watu 15 wameuawa baada ya kushambuliwa na waasi wa ADF wanaohusishwana kundi la Islamic State.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Mauaji hayo yametokea siku ya Ijumaa, katika vijiji vitatu, wilayani Lubero, baada ya waasi hao kutekeleza mashambulio hayo kwa mujibu wa viongozi wa kiraia na wakaazi.
Raia tisa waliuawa katika kijiji cha Kilonge, wawili Katanga na wanajeshi wawili katika kijiji cha Maendeleo, kwa mujibu wa Macaire Sivikunula, chifu wa eneo la Bapere, iliko vijiji hivyo.
ADF imeendelea kutekeleza mashambulio dhidi ya raia, mkoani Kivu Kaskazini, licha ya kuwepo kwa operesheni ya pamoja, iliyopewa jina shujaa, kati ya vikosi vya DRC na Uganda.
Wakati hayo yakijiri, Zambia siku ya Alhamisi wiki ijayo, itakuwa mwenyeji wa kikao cha Mawaziri wa Ulinzi kutoka nchi za eneo la Maziwa Makuu, kujadili hali ya utovu wa usalama, inayoendelea Mashariki mwa DRC.
Kikao hicho cha siku tatu, kinatarajiwa, kuthathmini kinachoendelea na nini nchi hizo za kikanda zinaweza kufanya kuzuia kuendelea kwa mapigano makali kati ya jeshi la DRC na waasi wa M23, wanaoungwa mkono na Rwanda, licha ya kuwepo kwa mkataba wa Washington, uliotiwa na viongozi wa DRC na Rwanda ili kusitisha mapigano.