
BAADA ya kurejea uwanjani akiwa fiti akitoka kuwa majeruhi, kiungo wa KMC, Ahmed Bakari ‘Pipino’ amesema huu ni muda mwafaka wa kuunganisha nguvu na wenzake kuipambania timu hiyo kuondoka mkiani.
KMC inaburuza mkia katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa inamiliki pointi nne kupitia mechi tisa, ikifunga mabao mawili, kushinda mechi moja na kupoteza saba na sare moja, kwa sasa ipo chini ya kocha mpya Abdallah Mohammed ‘Baresi’ baada ya kuachana na Mbrazili Marcio Maximo.
Pipino amesema kitendo cha timu hiyo kuzibeba 15 zilizopo katika ligi ikiwa ndio timu yenye pointi chache kinawanyima raha wachezaji, lakini wanaamini ligi itakaporejea kuanzia Januari 21 na kupata angalau ushindi wa mechi mbili zitawapa morali na kurudi katika mstari.
“Mechi mbili dhidi ya Pamba na Mtibwa Sugar kila moja nimecheza dakika 90 baada ya kupona kabisa majeraha. Ila ile ya Mbeya City sikuwa fiti kwani nilicheza kama dakika 65 au 70 nikatolewa. Lakini, kwa sasa nimefurahi kuungana na wenzangu kuipambania timu,” amesema na Pipino na kuongeza:
“Msimu umeanza kwa ugumu kwa timu na mimi binafsi, lakini bado nina muda wa kufanya vitu muhimu ambavyo vitafanya jina langu liendelee kutamkwa kwa ukubwa kama ilivyokuwa msimu uliopita.”
Pipino aliyemaliza msimu uliopita akiwa anawaniwa saini yake na Simba, Yanga na Azam kutokana na kuonyesha kiwango cha juu, amesema bado ana nafasi ya kucheza ndani na nje ya nchi na kwamba kikubwa kwake ni kupambana.
“Mimi ni mchezaji. Sio lazima hizo timu (tatu zilizokuwa zikimuwania) kinachotakiwa kwangu ni kuwa na mwendelezo wa kiwango (bora), ndio maana nasema kwa sasa nipo fiti na tayari kwa kazi,” amesema Pipino aliyewahi kuzitumikia timu za taifa kuanza za vijana hadi ile ya wakubwa.