WATAALAMU wa uchumi wametoa ushauri wa namna ya kukabiliana na hali ngumu ya kifedha mwezi Januari ikiwamo kuweka akiba mapema na kujiepusha na madeni mapya.
Pia, wameshauri kutumia kipato vizuri kwenye gharama za msingi wakati wa Januari ili kuepuka matumizi yasiyofaa.
Akizungumza na gazeti la HabariLEO, mtaalamu wa masuala ya uchumi, Walter Nguma alisema ni muhimu kupanga matumizi wakati wa sikukuu na kuacha akiba ya Januari kwa kuzingatia kipato chake.
Nguma alisema Januari watu wanapaswa kuangalia mbinu, mipango na njia mbadala ya kukabiliana na hali ngumu ya kiuchumi ili isiwe mzigo kwao na kuwatoa kwenye ‘reli’.
“Kipato cha Watanzania wengi zaidi ya asilimia 70 ni kwa ajili ya matumizi ya wakati huo, ni vizuri watu kuangalia kipato chao na mahitaji yanayohitajika hasa baada ya sikukuu kama ni watoto kwenda shule ili mwishoni usiwe na mzigo mkubwa,” alieleza Nguma.
SOMA: Wananchi wapongeza juhudi za Rais Samia kuwakwamua kiuchumi
Naye Mtaalamu wa Saikolojia, Elibariki Mkumbo alisema watu wengi wana mazoea ya kuweka malengo lakini wanashindwa kuendana na uhalisia wake, jambo linalowapa ugumu wa maisha hasa wakati huu ukiwa ni mwanzo wa mwaka.
“Watu wengi hawana ufahamu wa kuweka malengo lakini kuweka malengo bila mikakati hayawezi kufikika,” alisema Mkumbo.
Akizungumza kwenye kipindi cha Morning Trumpet cha televisheni ya Azam, mtaalamu wa uchumi Elisante Ephraim alisema ili kukabiliana na hali ngumu ya kifedha Januari, ni muhimu watu kutambua kipato chao na kuangalia mahitaji na gharama za lazima.
Alishauri watu kujiepusha na kukopa madeni mapya kutokana na msukumo usio wa lazima huku akiorodhesha madeni yaliyopaswa kulipwa na kuanza kulipa kwa awamu.
“Lazima kujua gharama za lazima mwezi huu ni zipi na unazipa kipaumbele kulingana na mahitaji yake kama chakula, malazi, ada za watoto na usafiri wa kwenda kazini.
Wakati huo hatushauri madeni mapya, Januari kuna mikopo mingi yenye riba kubwa sana,” alifafanua Ephraim.
Alisema Januari pia ni wakati mzuri wa kuanzisha biashara za kutoa huduma kuliko biashara za bidhaa zinazoweza kuchangia watu kukopa.
