AZAM FC inaendelea kujiimarisha katika maeneo mbalimbali ya kikosi hichona sasa imevamia Mlandege ya Zanzibar na kubeba mastaa wawili wa timu hiyo, akiwamo Aimar Hafidh Abubakar ‘Haaland’ na Suleiman Juma Kidawa ‘Pogba’ ambapo kocha Florent Ibenge aliwaambia mabosi wa klabu hiyo; ‘nileteeni hao fasta’.

Taarifa za usajili wa nyota hao zimevujishwa na rafiki yao wa karibu aliyesimulia mwanzo mwisho ilivyokuwa.

“Haaland amesaini Azam jana (juzi) Jumamosi usiku na kesho Jumatatu (leo) pia Pogba anaweza kusaini kwani tayari mazungumzo yamefanyika, akaambiwa ajiandae muda wowote jambo litakuwa freshi.

“Usajili wa Haaland ulikuwa wa haraka sana, baada ya mechi yetu ya kwanza katika Mapinduzi dhidi ya Singida Black Stars na mshambuliaji huyo kupewa tuzo ya mchezaji aliyeonyesha mchezo wa kiungwana huku akicheza vizuri sana, mabosi wa Singida Black Stars walimfuata, wakazungumza naye lakini wakashindwana.

AZA 01

“Tulipokuja kucheza na Azam, baada ya mechi kocha Ibenge alimfuata Haaland na Pogba akazungumza nao kwamba anawahitaji kikosini kwake,” amesema mtu huyo.

Aliongeza, dili la Haaland lilikamilika baada ya Mtendaji Mkuu wa Azam, Octavi Anoro akiongozana na Abdulkadir Seif ‘Qudabash’ kufika Uwanja wa Mao wakati Mlandege ikicheza mechi ya kirafiki dhidi ya TRA United juzi jioni, na kuondoka naye.

“Jana (juzi) Jumamosi kulikuwa na mechi ya Mlandege na TRA kwenye Uwanja wa Mao, akaja bosi wa Azam yule Mzungu (Anoro) na jamaa anayeongozana naye (Qudabash), wakafanya mazungumzo na bosi wa Mlandege, Haaland akaitwa akapakiwa kwenye gari wakaondoka naye,” amesema.

Katika usajili wa dirisha kubwa msimu huu, Simba iliwahi kuelezwa kumhitaji Pogba, baadaye TRA United ikaingilia kati na kumtumia mkataba, lakini dili hilo halikufanikiwa baada ya kushindwana katika maslahi.

AZA 02

Mbali na nyota hao wa Mlandege, Azam pia imemalizana na kiungo mshambuliaji wa KMKM, Mzee Hassan Mzee maarufu Aziz KI ambaye tayari amepelekwa timu ya vijana.

Licha ya kwamba usajili huo ndio umefichuliwa hivi karibuni, lakini inaelezwa Azam ilimalizana naye mapema sana na tayari ameshafika viunga vya Chamazi jijini Dar.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *