
KOCHA Mkuu wa Mtibwa Sugar, Yusuf Chipo amelia na safu ya ulinzi kurudia makosa, huku akisisitiza wamekutana na timu bora ambayo imetumia udhaifu walionao kuwaadhibu na sasa wanaenda kujipanga kwa mechi zijazo za duru la pili la Ligi Kuu Bara.
Mtibwa ilikumbana na kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa Singida Black Stars, kikiwa ni cha pili mfululizo kwao tena wakiwa kwenye uwanja wa nyumbani, kwani mechi iliyopita pia ililala kwa idadi hiyo mbele ya Mashujaa. Mtibwa inautumia Uwanja wa Jamhuri, Dodoma kama wa nyumbani baada ya Manungu Complex, kufungiwa.
Akizungumza na Mwanaspoti, Chipo amesema licha ya kufanyia kazi upungufu katika safu ya ulinzi, makosa hayo yamejirudia tena na kuongeza rekodi mbaya ya kufungwa mabao mengi ndani ya mechi moja.
“Sijafurahishwa na matokeo hayo, nitarudi kwenye uwanja wa mazoezi kusawazisha makosa kabla ya kuikabili Azam FC katika mechi ijayo,” amesema Chipo ambaye ni raia wa Kenya na kuongeza;
“Kufungwa mabao zaidi ya mawili katika mechi moja inaumiza sana huu ni mchezo wa pili kwenye ligi tunarudia makosa, nitakaa na wachezaji wangu kujua shida ni nini kabla ya kuifuata Azam FC ugenini katika mchezo unaofuata.
“Tunaenda kukutana na timu nyingine bora kama ilivyo kwa Singida, wachezaji wakifanya makosa wanaadhibiwa na sitamani kuona timu inarudia makosa tena. Nitafanyia kazi dosari zote nilizoona, ili kuhakikisha tunakuwa bora na kupata pointi tatu muhimu.”
Chipo amesema kwa ujumla juzi hawakuwa bora katika idara zote, kuanzia kushambulia hadi kuzuia na wameadhibiwa na mbinu bora kutoka kwa wapinzani wao, lakini wanajipanga kusawazisha makosa ili warudi wakiwa imara na hatimaye kurudisha ushindani.
“Tunatambua tutakuwa na dakika 90 nyingine ngumu na za ushindani kutoka kwa Azam kutokana na ubora wa mpinzani, nasi tunatakiwa kujiandaa na kushindana, ili kurudisha ubora wetu hasa baada ya kutoka kupoteza kwa idadi kubwa ya mabao tukiwa kwenye uwanja wa nyumbani,” amesema Chipo na kuongeza;
“Ligi ni ngumu kila timu inapambana kusaka ushindi na ili kuweza kuendana na kasi iliyopo ni kuhakikisha hatufanyi makosa. Tunaiheshimu Azam FC ni timu nzuri ina wachezaji wengi bora na wazoefu na sisi hatutaki kurudia makosa tunatarajia mchezo bora na wa ushindani Jumatano hii.”
Mtibwa imecheza mechi 15 ikikusanya pointi 21 baada ya kushinda tano, sare sita na kupoteza nne, huku ikifunga mabao 13 na kuruhusu mabao 14. Inashika nafasi ya tano ikishushwa na Simba ilitoka kuinyoa TZ Prisons kwa mabao 2-0 juzi usiku kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma.