
Marekani inasema haina mpango wa kuikalia nchi hiyo ya Amerika Kusini. Guterres aliyasema hayo katika taarifa iliyowasilishwa katika Mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama na mkuu wa masuala ya kisiasa wa Umoja wa Mataifa Rosemary DiCarlo. “Ninatoa wito kwa wahusika wote wa Venezuela kushiriki katika mazungumzo jumuishi na ya kidemokrasia ambapo sekta zote za jamii zinaweza kuamua mustakabali wao. Pia ninawasihi majirani wa Venezuela, na jumuiya ya kimataifa kwa upana zaidi, kuchukua hatua ya mshikamano na kwa kuzingatia misingi, sheria na kanuni zilizowekwa ili kukuza mazingira ya kuishi kwa amani.”
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Mike Waltz aliliambia Baraza la Usalama kwamba Marekani ilifanya “operesheni mahsusi ya utekelezaji wa sheria iliyoendeshwa na jeshi la Marekani dhidi ya watuhumiwa wawili wanaosakwa na Marekani,” akimaanisha Maduro na mkewe Cilia Flores. Naye Balozi wa Venezuela Samuel Moncada, aliita operesheni hiyo kuwa ni “shambulio haramu la silaha” lisilo na uhalali wowote wa kisheria.
Baraza la Usalama lenye nchi wanachama 15 lilikutana katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa huko New York saa chache tu kabla ya Maduro kufikishwa katika mahakama ya shirikisho ya Manhattan. Alishitakiwa kwa mashtaka ya dawa za kulevya ikiwa ni pamoja na njama za ugaidi unaosababishwa na dawa za kulevya. Maduro amekanusha mashitaka dhidi yake.