NAIBU Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew ametembelea mradi wa maji wa miji 28 wilayani Serengeti na kuagiza ndani ya siku 60 kilometa 30 za mtandao wa mabomba ziwe zimekamilika.

Kundo amesema haridhishwi na maendeleo ya mradi huo ambao ulitarajiwa kukamikika Aprili 2025.

Amesisitiza kuwa serikali haidaiwi na imekuwa ikitoa fedha kwa wakati jambo ambalo lilitarajiwa kuwezesha mradi kukamilika.

Amebainisha baadhi ya upungufu kwa mkandarasi kuwa ni pamoja na kuwa na wafanyakazi wachache kulinganisha na mkataba huku wengine wakiwa hawana sifa, kushindwa kununua vifaa kwa wakati na pia kutokulipa wafanyakazi kwa wakati.

Kufuatia upungufu huo amemuagiza mkandarasi kampuni ya Mega Engeneering and Infrastructure Company Ltd kuongeza wafanyakazi na kuwasilisha orodha ya wafanyakazi wote ofisi ya Mkuu wa Wilaya na pia malipo yao ya kila mwezi ili kuondoa manunguniko.

Pia ameagiza mkandarasi kuhakikisha ndani ya siku 14 vifaa vyote vinavyohitajika kufanyia kazi viwe vimewasili.

Aidha Kundo amemtaka mkandarasi mkuu ndani ya siku tatu afike katika kikao kwa mazingumzo na maagizo ya kina.

Mradi wa maji wa miji 28 Wilayani Serengeti unatekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 21 na unatarajia kuhudumia wananchi wapatao 166,000.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *