
Nicolás Maduro amejitangaza kuwa “rais halali wa Venezuela” wakati alipokuwa akipinga kukamatwa kwake na amekanusha mashtaka ya usafirishaji wa dawa za kulevya, mashtaka ambayo utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump ulitumia kuhalalisha kuondolewa kwake madarakani.
Akiwa mahakamani, Maduro alisema kwa lugha ya Kihispania – kupitia mkalimani kwamba “alikamatwa”, kabla ya jaji kumkatiza.
Alipoulizwa msimamo wake kuhusu mashtaka yanayomkabili, Maduro alisisitiza kuwa hana hatia, ni mtu mwadilifu, na kwamba bado yeye ndiye rais halali wa nchi yake.
Hii ilikuwa ni mara yake ya kwanza kufikishwa mahakamani Manhattan tangu yeye na mkewe, Cilia Flores, walipokamatwa nyumbani kwao Caracas Jumamosi katika operesheni ya kijeshi ya kushtukiza. Flores pia amekana mashtaka.
Maduro, mwenye umri wa miaka 63, alifikishwa mahakamani chini ya ulinzi mkali mapema Jumatatu – alisafirishwa kwa helikopta hadi Manhattan kutoka Brooklyn, ambako amekuwa akizuiliwa na kisha kupelekwa mahakamani kwa gari maalum lenye ulinzi mkali. Akiwa pamoja na mkewe, waliwasili mahakamani dakika chache kabla ya saa sita mchana.
Maandamano ya kuonyesha mshikamano na Maduro
Wote walikuwa wamefungwa pingu za miguu na kuvalishwa mavazi ya gerezani, walitumia vinasa sauti ili kufuatilia mwenendo wa kesi iliyoendeshwa kwa lugha ya Kiingereza na kutafsiriwa kwa Kihispania.
Jaji ameagiza wote wawili wabaki rumande na ametangaza tarehe mpya ya kusikilizwa kwa kesi hiyo kuwa Machi 17.
Kukamatwa kwa Nicolas Maduro kumetajwa na wachambuzi kama tukio lisilo la kawaida katika historia ya mahusiano ya kimataifa, kwani ni nadra kwa kiongozi wa taifa kufikishwa mahakamani nchini Marekani kwa mashtaka ya uhalifu wa kimataifa.
Wakati huo huo nchini Venezuela, maelfu ya watu waliandamana hasa katika mji mkuu Caracas kama ishara ya kumuunga mkono Maduro huku naibu wake wa zamani Delcy Rodqriguez, akiapishwa kuwa rais wa muda.
Kwa mujibu wa mfumo wa kisheria wa Marekani, kama mshtakiwa wa jinai, Maduro atakuwa na haki sawa na mtu mwingine yeyote anayekabiliwa na mashtaka ya uhalifu nchini humo—ikiwemo haki ya kusikilizwa na baraza la waamuzi.
Hati ya mashtaka ya kurasa 25 inamtuhumu Maduro na washirika wake kushirikiana na magenge ya dawa za kulevya kusafirisha maelfu ya tani za Cocaine kuingia Marekani. Maduro anakabiliwa na kifungo cha maisha endapo atapatikana na hatia.
Miongoni mwa makosa mengine, hati ya mashtaka inawashutumu Maduro na mkewe kwa kuagiza utekaji nyara, vipigo na mauaji ya watu waliowadai fedha za dawa za kulevya au waliodhaniwa kuhatarisha operesheni ya usafirishaji wa dawa hizo.
Kabla ya kukamatwa kwake, Maduro na washirika wake walidai kuwa uhasama wa Marekani unatokana na tamaa ya rasilimali za mafuta na madini za Venezuela.
Kiongozi mpya wa mpito wa Venezuela, Delcy Rodríguez, ametoa mwito kwa Marekani kumrudisha Maduro nyumbani ambaye kwa muda mrefu amekana kuhusika na ulanguzi wa dawa za kulevya.
Rodríguez mnamo siku ya Jumapili, alionekana kuonyesha msimamo wa maridhiano zaidi katika chapisho la mitandao ya kijamii, akihimiza ushirikiano na Trump na “uhusiano wa heshima” na Marekani.