DAKIKA 90 za beki mpya ndani ya Simba, Charles Ouma Sila, kwa kiasi fulani zimempa matumaini kocha mkuu wa kikosi hicho, Steve Barker, lakini amebainisha kwamba anahitaji muda kidogo kufanya uamuzi juu ya mchezaji huyo.

Sila yupo na kikosi cha Simba kinachoshiriki Kombe la Mapinduzi 2026 kikiwa kimefuzu nusu fainali na kesho Alhamisi kitashuka dimbani kukabiliana na Azam.

Beki huyo mwenye asili ya Kenya akiwa na uraia wa Sudan Kusini, juzi wakati Simba inaichapa Fufuni mabao 2-1 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja na kufuzu nusu fainali, alizima mwanzo mwisho sambamba na Vedastus Masinde, huku Chamou Karaboue na Rushine De Reuck waliocheza mechi ya kwanza dhidi ya Muembe Makumbi City wakikosekana. Chamou aliishia benchi, wakati Rushine akitupwa jukwaani kabisa.

Beki huyo ambaye ametokea Kenya Police inayoshiriki Ligi Kuu ya Kenya, kuna vitu vitatu vinambeba na huenda vikampa ulaji ndani ya Simba ambavyo ni utulivu, matumizi ya mguu wa kushoto na kimo chake kirefu, ingawa anahitaji kuongeza kasi.

Chanzo kutoka ndani ya kambi ya Simba iliyopo Unguja, kimesema kuanzia mazoezini, beki huyo amekuwa akifanya vizuri huku nafasi aliyopewa kucheza dhidi ya Fufuni, imezidi kumuongezea sifa za kubaki kikosini.

Mtoa taarifa huyo amesema kocha Barker katika kukifanyia tathmini kikosi chake, ametaka kumuona zaidi beki huyo iwe mazoezini au katika mechi kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho wa kupewa mkataba au kutosajiliwa.

“Sila alicheza vizuri na hadi kocha alimsifia kutokana na utulivu wake kwenye ulinzi licha ya kwamba hana muda mrefu tangu aje Simba.

“Anafanya majaribio na mambo yakienda vizuri huenda akasajiliwa kutokana na upekee alionao tofauti na mabeki wa kati waliopo sasa. Upekee huo ni matumizi yake ya mguu wa kushoto kwani Simba mabeki wa kati waliopo wote wanatumia miguu ya kulia,” kilisema chanzo hicho.

“Kingine ni mtulivu. Mechi ya kwanza amecheza sambamba na Masinde (Vedastus) lakini wamekuwa imara licha ya kuruhusu bao moja. Jambo la tatu ana umbo la beki wa kati. Ni mrefu,” kimefichua chanzo hicho.

Ndani ya Simba hivi sasa, mabeki wa kati ni Chamou Karaboue, Rushine De Reuk, Vedastus Masinde na Abdulrazak Hamza ambao wote hao wanatumia mguu wa kulia.

Katika soka la kisasa, makocha wengi hupendelea beki wa kati mmoja awe anatumia mguu wa kushoto ili akicheza asaidiane na beki wa upande wa kushoto kuzuia mashambulizi kwa urahisi yakipitia upande huo.

Hata hivyo, kumekuwa na taarifa kwamba huenda Chamoue akaachwa na Simba kwa sababu mbalimbali ikiwemo kuwa na makosa mengi, kama sio sasa kipindi cha dirisha dogo, basi mwisho wa msimu mkataba wake utakapomalizika.

Kwa sas Abdulrazak Hamza anauguza majeraha hali inayofanya Simba kubakiwa na mabeki wa kati watatu, Chamoue na Rushine wanaocheza mara kwa mara, huku Masinde aliyesajiliwa msimu huu akiwa hajacheza mechi yoyote.

 Akizungumzia kiwango cha Sila na nyota wengine wa Simba, Barker amesema: “Ninafurahishwa na maendelo ya wachezaji siku hadi siku, tunaendelea kuwaangalia kuona tunajenga vipi kikosi chetu kwa ajili ya mashindano yaliyo mbele yetu.”

Kwa mujibu wa mtu mmoja wa benchi la ufundi la Simba amedokeza kwamba Barker anapenda mchezaji mwenye utayari wa kutumika katika nafasi zaidi moja kwani hiyo inatoa machaguo tofauti kulingana na mwenendo wa msimu kutokana na wakati mwingine timu inaweza kupoteza mchezaji muhimu, hivyo kwa sasa anaangalia kwa umakini wachezaji waliopo wanafiti kwa namna gani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *