NDANI ya Yanga, kuna mchakato wa kusajili straika na Mwanaspoti linafahamu kwamba Kocha Pedro Goncalves tayari amewasilisha jina la mtu anayemhitaji.
Kati ya majina ambayo Mwanaspoti linafahamu mojawapo litasainiwa Yanga kuongeza nguvu eneo la ushambuliaji ni Laurindo Dilson Maria Aurelio ‘Depu’ anayeitumikia Radomiak Radom ya Poland kwa mkopo akitokea Vojvodina ya Serbia.
Mwingine ni Jacinto Muondo ‘Gelson’ Dala anayeitumikia Al-Waktah ya Qatar akitokea Rio Ave ya Ureno. Wote ni raia wa Angola na mmoja kati yao atavaa jezi za Yanga wiki chache zijazo.
Akizungumzia mipango ya kusajili straika baada ya kuondoka Andy Boyeli ambaye amerejea Sekhukhune United ya Afrika Kusini baada ya Yanga kumchukua kwa mkopo akitumika kwa miezi sita pekee, Pedro amesema mpango huo upo ili kuongeza nguvu eneo hilo.
Pedro amesema wanalazimika kusajili straika wa kati kusaidiana na Prince Dube kipindi hiki ambacho Clement Mzize anarejea taratibu kutoka kwenye majeraha.
Mreno huyo amegusia kwamba, hata ujio wa Emmanuel Mwanengo ni sehemu ya maboresho ya eneo la ushambuliaji kutokana na uwezo alionao wa kucheza mshambuliaji wa kati na kutokea pembeni.
Baada ya kumshuhudia Mwanengo akimaliza dakika tisini akisimama mshambuliaji wa kati Yanga iliposhinda 3-0 dhidi ya KVZ katika Kombe la Mapinduzi, Januari 4, 2026, huku nyota huyo mpya akihusika katika bao la tatu, Pedro amesema: “Ana ujuzi wa kucheza kama winga na mshambiaji, kiwango alichoonyesha kimenifurahisha ingawa pengine ni uchovu umemfanya asifanye kwa kiwango kikubwa zaidi. Ninajua huenda hiyo si nafasi yake ya kwanza, lakini tunapaswa kuwa wawazi, na yeye pia yuko tayari kujaribu nafasi hizo na kucheza dakika 90.”
Pedro aliongeza: “Kwa sasa Dube amemaliza majukumu ya AFCON, hivyo tumempa siku saba za kupumzisha mwili na akili. Ni muhimu kwa sababu tulikuwa tumemsukuma sana. Kwa hiyo, nilikusanya nguvu zote kwa kuwa msimu utakuwa mgumu sana. Na pia, sasa mambo yanaenda vizuri zaidi kwani yuko katikati ya mchakato.
“Lakini katika kuimarisha kikosi, tunafanya kazi ya kusajili mshambuliaji mwingine. Kwa sasa Mzize yupo nje akiwa bado hajapona vizuri.”
Baada ya kuondoka Boyeli aliyefunga mabao mawili kwenye ligi, mshambuliaji aliyebaki Yanga ni Dube na Mzize ambaye anarejea taratibu kutoka kwenye majeraha. Hali hiyo imefanya mabosi wa Yanga kumsajili Mwanengo kutoka TRA United akiwa na uwezo wa kucheza nafasi zote za ushambuliaji.