
Serikali ya Burkina Faso imejieleza kuhusu jaribio la mapinduzi la hivi karibuni, ambalo lilishindwa Jumamosi, Januari 3. Katika mahojiano yaliyorushwa kwenye televisheni ya umma, Waziri wa Usalama ameeleza kwamba wahusika wa jaribio hili walikuwa wamepanga mauaji ya Kapteni Ibrahim Traoré na wanajeshi na raia kadhaa.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Watu kadhaa wamekamatwa kuhusiana na njama hii, ambayo serikali ya Burkina Faso inadai iliongozwa na rais wa zamani wa mpito Paul-Henri Sandaogo Damiba kwa fedha kutoka Côte d’Ivoire.
Kulingana na Waziri wa Usalama Mahamadou Sana katika taarifa yake, operesheni ya kuhatarisha usalama wa taifa ilipangwa kufanyika Jumamosi, Januari 3, saa 5:00 usiku na ingelihusisha mfululizo wa mauaji ya wanajeshi na raia, “kuanzia na mauaji ya rafiki na Kapteni Ibrahim Traoré.” “Kitendo hiki kilipaswa kufuatiwa na operesheni ya kuvunja kambi ya ndege zisizo na rubani na uingiliaji kati wa kijeshi wa ardhini na vikosi vya nje,” ameogeza.
Kwa serikali ya Burkina Faso, mtu anayehusika na jaribio hili jipya la kuhatarisha usalma ni afisa wa zamani wa cheo cha Luteni Kanali Paul-Henri Sandaogo Damiba, rais wa zamani wa serikali ya mpito. Amekuwa uhamishoni nchini Togo tangu mapinduzi yaliyomwondoa madarakani mnamo mwezi Septemba 2022 na kumleta Ibrahim Traoré madarakani.
“Dhamira yake muhimu ilikuwa kubuni na kupanga vitendo, kutafuta na kuhamasisha fedha, na kuajiri raia na wanajeshi,” Mahamadou Sana amesema. “Jeshi lilipewa jukumu la kuwashirikisha wanajeshi wengine na kuanzisha vikundi vya vitendo vyenye misheni zilizoainishwa wazi. Na raia walipaswa kuhamasisha wafuasi wao ili, baada ya hatua ya kijeshi, waweze kuhamasisha wafuasi wao wenyewe na kuunga mkono operesheni ya kijeshi.” “Hakuna majina mengine yaliyotajwa, ‘ili kutoathiri uchunguzi unaoendelea,’ waziri amesema. Video ilitolewa ambapo mmoja wa waendeshaji biashara wanaodaiwa kuhusika katika jambo hilo “anakiri”, akielezea jukumu lake na hatua zilizopangwa katika operesheni hii ya kuhatarisha usalama wa taifa.
Hatimaye, Waziri Mahamadou Sana ameongeza kwamba ‘sehemu kubwa’ ya ufadhili wa jaribio hili la mapinduzi ilianzia Côte d’Ivoire na ilihusisha uhamisho wa faranga milioni 70 za CFA.”