Waziri wa mambo ya nje wa Israel Gideon Saar ameahidi kwamba nchi yake itakuza uhusiano wenye mafanikio na Somaliland baada ya kuwa nchi ya kwanza kutambua uhuru wa eneo hilo lililojitenga na Somalia.

Katika ziara yake ya kwanza rasmi Somaliland, Saar amesema Israel itafungua ubalozi hivi karibuni mjini Hargeisa na kumteua balozi atakayewakilisha nchi hiyo ndani ya ardhi ya Somaliland, licha ya ukosoaji mkubwa wa kimataifa kuhusu uamuzi wake wa kulitambua eneo hilo, ambalo sehemu kubwa ya dunia inalichukulia kuwa sehemu ya Somalia.

Kwa mujibu wa nakala ya hotuba iliyoonekana na shirika la habari la AP, mwanadiplomasia huyo amesisitiza kuwa hakuna taifa litakaloielekeza Israel kuhusu nani wa kumtambua au nchi gani idumishe nayo uhusiano wa kidiplomasia.

Saar amesema uamuzi huo ni sehemu ya sera huru za Israel katika kutafuta ushirikiano wa kimkakati duniani.

Somalia yakasirishwa na ziara ya Gideon Saar Somaliland

Rais wa Somaliland Abdirahman Mohamed Abdullahi ameeleza kuwa ziara ya Saar “ina umuhimu wa kihistoria na kuashiria mwanzo wa enzi mpya ya ushirikiano” kati ya nchi hizo mbili.

Kiongozi huyo ameusifu uamuzi wa Israel aliouita wa kijasiri, akieleza kwamba utafungua fursa pana za kiuchumi na maendeleo.

 “Unakuza ushirikiano wa maslahi ya kimkakati kati ya nchi hizo mbili,” Abdullahi amesema katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Somaliland Abdirahman Dahir Adan katika mahojiano na shirika la habari la AP amesema nchi yake inatoa mkono wa shukrani kwa kutambuliwa rasmi na Israel.

Ameongeza kuwa Israel na Somaliland ni washirika wa kiasili, kwa kuwa nchi zote zinakabiliwa na uhasama kutoka kwa mataifa jirani na zina maslahi ya pamoja katika suala la usalama wa Bahari ya Sham – eneo muhimu kwa biashara ya kimataifa na usafirishaji wa mafuta.

Adan ametabiri kuwa mataifa mengine yatafuata mfano wa Israel na kuitambua Somaliland kama nchi huru katika siku zijazo.

Ufafanuzi: Somaliland ni taifa huru?

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Hata hivyo Somalia imeonekana kukasirishwa na ziara ya Gideon Saar, ikiitaja ziara hiyo kama “uvamizi haramu” na “usioidinishwa.”

Katika taarifa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Somalia imesema “inahifadhi haki ya kuchukua hatua zote zinazofaa za kidiplomasia na kisheria ili kulinda mamlaka yake, umoja wa kitaifa na uadilifu wa eneo lake.”

Somalia imekuwa ikisisitiza kwa miaka mingi kwamba Somaliland ni sehemu isiyotenganishwa ya ardhi yake, na hatua yoyote ya kuitambua inakiuka sheria za kimataifa kuhusu mipaka ya mataifa.

Mkutano maalum wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika uliofanyika jana Jumanne umelaani vikali uamuzi wa Israel wa kuitambua Somaliland na kuhimiza uamuzi huo “ufutwe mara moja.”

Hata hivyo uamuzi wa Israel umeuungwa mkono na Marekani, japo umekosolewa na Misri, Uturuki, Baraza la Ushirikiano la Ghuba lenye nchi sita, pamoja na Shirika la Ushirikiano wa Kiislamu lenye makao makuu yake Saudi Arabia. Umoja wa Ulaya umesisitiza kuwa mamlaka ya Somalia yanapaswa kuheshimiwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *