Ingawa Saudi Arabia na UAE kwa muda mrefu zimekuwa washirika, tukio hilo limeibua maswali mapya: ni mkakati upi wa sera za kigeni una nafasi kubwa ya kudumu na kufanikiwa katika eneo lenye migogoro mingi ya Mashariki ya Kati?

Kwa miaka mingi, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabuzimekuwa zikishindana kimyakimya katika ushawishi wa kikanda. Hata hivyo, wiki iliyopita ushindani huo ulibadilika na kuwa uhasama wa wazi na wa kijeshi. Mnamo Desemba 30, Saudi Arabia ilifanya shambulio la anga katika mji wa bandari wa Mukalla nchini Yemen, ikilenga shehena ya silaha zilizokuwa zikielekezwa kwa wanamgambo wa kujitenga kusini mwa nchi hiyo.

Silaha hizo ziliripotiwa kutumwa na UAE kwa ajili ya Baraza la Mpito la Kusini, STC, ambalo linataka kuanzisha taifa huru kusini mwa Yemen. UAE ilikanusha madai hayo, ikisema silaha hizo zilikuwa kwa ajili ya vikosi vyake vya usalama vilivyoko eneo hilo. Hata hivyo, Saudi Arabia ilisema ilikuwa imetoa onyo mapema na ikaeleza kuwa hatua za UAE zilikuwa hatari sana kwa usalama wa kikanda.

Muungano wa Saudia wakataa kusitisha mapigano Yemen

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Mkoa wa Hadramout, ambako STC inaendesha shughuli zake, unapakana moja kwa moja na Saudi Arabia. Kwa Riyadh, uwepo wa kundi lisilo rafiki karibu na mpaka wake ni jambo lisilokubalika. Mashambulizi hayo yalikuwa mara ya kwanza kwa Saudi Arabia na UAE kukabiliana moja kwa moja kijeshi. Baada ya tukio hilo, UAE ilitangaza kuondoa wanajeshi wake waliosalia nchini Yemen. Hata hivyo, wachambuzi wanasema mgogoro huu una mizizi mirefu zaidi, inayotokana na mitazamo miwili tofauti ya sera za kigeni.

Saudi Arabia, kwa sasa, inaonekana kujikita zaidi katika utulivu wa kikanda, ushirikiano wa kiuchumi, maendeleo ya ndani, na matumizi ya taasisi za kimataifa kama Umoja wa Mataifa. Kinyume chake, UAE imekuwa ikituhumiwa kufuata mkakati wa kuunga mkono makundi yasiyo ya kiserikali ili kujenga ushawishi wake bila kutegemea serikali rasmi.

Kwa mujibu wa wachambuzi wa masuala ya usalama, UAE imekuwa ikiunda kile kinachoelezwa kama “mhimili wa wanaotaka kujitenga,” kwa kusaidia makundi yenye silaha katika nchi kama Libya, Sudan, Somalia na Yemen — madai ambayo Abu Dhabi imekuwa ikiyakanusha mara kwa mara.

Yemen Seiyun 2026 | Mashambulizi ya anga dhidi ya vikosi vya Baraza la Mpito la Kusini kusini mwa nchi
Mashambulizi ya anga dhidi ya vikosi vya Baraza la Mpito la Kusini kusini mwa nchiPicha: Aden Independent Channel (AIC TV)/AFP

Kupitia mtandao mpana wa kifedha, usafirishaji, vyombo vya habari na bandari, UAE imefanikiwa kujipatia ushawishi mkubwa katika njia muhimu za biashara na nishati, hasa katika Bahari ya Sham na Ghuba ya Aden. Hali hii imeziweka Saudi Arabia na UAE katika pande tofauti za migogoro mbalimbali.

Sudan ni mfano mmoja, ambako Saudi Arabia inaunga mkono serikali inayotambuliwa kimataifa, huku UAE ikituhumiwa kusaidia vikosi vya RSF. Vilevile, Saudi Arabia imepinga hatua ya Israel kuitambua Somaliland, wakati UAE imekaa kimya, ikizingatiwa uhusiano wake wa karibu na Israel na Somaliland.

Licha ya mivutano hii, wachambuzi hawaoni uwezekano wa mgogoro mkubwa wa wazi kati ya mataifa hayo mawili. Badala yake, wanaeleza kuwa kinachoendelea ni aina ya “vita baridi” ya kisera. Kwa sasa, inaonekana Saudi Arabia na UAE kila moja itaendelea kushikilia mkondo wake wa sera za kigeni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *