Iran iko chini ya shinikizo la kimataifa baada ya rais wa Marekani Donald Trump kutishia kutumia nguvu za kijeshi kuwaokoa waandamanaji iwapo maafisa wa usalama wa Iran wataendelea kuwafyatulia risasi waandamanaji.
Kauli ya Trump imetolewa miezi saba baada vikosi vya Israel na Marekani kuvishambulia kwa mabomu vinu vitatu vya nyuklia vya Iran katikati ya mwezi Juni mwaka jana katika vita vilivyodumu siku 12. Israel nayo ilisema wiki iliyopita kwamba inasimama pamoja na waandamanaji wa Iran.
Kauli kama hizi zimepelekea kiongozi wa juu ya Iran Ayatolla Ali Khamenei kuapa kutowakinga maadui wa taifa lake huku Jaji Mkuu Gholamhossein Mohseni Ejei, akisema kufuatia matamshi ya Israel na Marekani, hakuna sababu ya mtu yeyote kuingia barabarani kwa maandamano na kufanya vurugu.
Amesema kuanzia hii leo hakutakuwa na uvumilifu wa aina yoyote kwa wale wanaowasaidia maadui wa Iran na kuvuruga utulivu wa watu wa taifa hilo. Kamanda wa jeshi la Iran pia ametoa tamko kuhusiana na yanayojiri nchini humo. Jenerali Amir Hatami ameonya kuwa Tehran haitovumilia vitisho kutoka nje.
Amesema Iwapo adui wa taifa hilo atafanya kosa kuivamia Iran majibu yake yatakuwa makali kushinda yale ya Juni 12.
“Leo hakuna shaka kuhusu uadui wa rais wa Marekani na waziri mkuu mhalifu wa Israeli dhidi ya taifa la Iran. Wanajiingiza katika mambo yetu ya ndani. Wanaandika mitaandaoni, wanazungumza. Wamekuwa adui zetu katika historia yetu yote. Na miezi sita au saba iliyopita waliwaua zaidi ya Wairani 1000, wakiwemo makamanda, wanajeshi, wanasayansi, watoto, wasichana na wavulana”, alitahadharisha Hamati.
Maandamano yageuka kuwa ya kisiasa
Takriban watu 27 wameuawa na zaidi ya 1,500 wamekamatwa ndani ya siku 10 za mwanzo za maandamano huku watu wengi zaidi wakijeruhiwa upande wa Magharibi wa taifa hilo. Kulingana na mtandao wa wanaharakati wa kutetea haki za binaadamu wa HRANA watu 36 waliuawa huko huku wengine zaidi ya 2000 wakikamatwa.
Maandamano hayo makubwa ambayo hayajawahi kushuhudiwa ndani ya miaka mitatu nchini humo, yalianza mwezi uliopita yakiwahusisha wauza maduka waliolalamika kuhusu kushuka kwa thamani ya fedha za taifa hilo.
Maandamano hayo sasa yamegeuka na kuwa ya kisiasa kupinga kudorora kwa uchumi, kupanda kwa gharama ya maisha wakidai hali hiyo imesababishwa na sera mbovu za rais Masoud Pezeshkian na vikwazo vya kiuchumi ilivyowekewa nchi hiyo na mataifa ya Magharibi. Kubanwa kwa uhuru wa kijamii na kisiasa pia ni mambo yanayowakasirisha waandamanaji.
Hata hivyo Rais Pezeshkian ametoa amri kwa vikosi vya usalama kutowakamata waandamanaji akiwatofautisha waandamanaji wa amani na wale wanaozua vurugu.
Naibu rais wa Iran Mohammad Jafar Ghaempanah amesema wale waandamanaji waliojihami kwa silaha kwa mfano visu na marungu na wale wanaoshambulia vituo vya polisi na maneo ya kijeshi hao watakabiliwa vikali.
Wachambuzi wanasema hatua ya Pezeshkian inaonesha wazi kwamba serikali inawasiwasi kwamba maandamanao yanaweza kuwa makubwa na kutoka nje ya uwezo wa serikali kuyadhibiti.