Denmark na Greenland wanatafuta mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, baada ya serikali ya Marekani kusisitiza kwa mara nyingine nia yake ya kutaka kuidhibiti Greenland — kisiwa cha eneo la Aktiki kinachomilikiwa na Denmark.
Mvutano umeongezeka baada ya Ikulu ya Marekani kusema kuwa daima inaweza “kuzingatia matumizi ya kijeshi,” hata wakati viongozi mbalimbali wa Ulaya wakipuuzia madai hayo mapya ya Marekani ya kutwaa kisiwa hicho kwa sababu za kimkakati.
Waziri Mkuu wa Denmark, Mette Frederiksen, alionya kwamba jaribio la Marekani kuchukua Greenland lingeweza kuhatarisha uhai wa muungano wa kijeshi wa NATO. Viongozi wa mataifa ya Ufaransa, Ujerumani, Italia, Poland, Uhispania na Uingereza waliunga mkono kauli ya Frederiksen kusisitiza kuwa kisiwa hicho chenye utajiri wa madini ni mali ya Denmark. Kauli hiyo ilisisitiza uhuru wa Greenland, kisiwa kinachojitawala lakini bado ni sehemu ya Ufalme wa Denmark na mwanachama wa NATO.
Tangu muhula wake wa kwanza, Rais wa Marekani Donald Trump amekuwa akijadili wazo la kununua au kuimiliki Greenland akidai kuwa Marekani inahitaji kudhibiti kisiwa hicho kikubwa zaidi duniani kwa ajili ya usalama wake, hasa kutokana na ushindani unaoongezeka kutoka China na Urusi katika eneo la Aktiki.
Operesheni ya kijeshi ya Marekani iliyofanyika Caracas mwishoni mwa wiki imeongeza wasiwasi barani Ulaya, na viongozi wa Marekani wameendelea kusisitiza kuwa wanataka udhibiti wa Greenland, ambayo iko katika eneo la kimkakati linalolinda njia za Aktiki na Atlantiki ya Kaskazini kuelekea Marekani.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Denmark, Lars Løkke Rasmussen, pamoja na mwenzake wa Greenland, Vivian Motzfeldt, wameomba kukutana na Rubio hivi karibuni. Wamesema maombi yao ya awali hayakufanikiwa.
Huku wanasiasa wengi wa chama cha Republican wakimuunga mkono Rais wa Marekani, baadhi ya maseneta wa pande zote mbili za siasa—Jeanne Shaheen na Thom Tillis—walikosoa vikali kauli ya kutaka kuitwaa Greenland. Walisema kwamba ikiwa Denmark na Greenland wameweka wazi kuwa kisiwa hicho hakitauzwa, Marekani inapaswa kuheshimu makubaliano yake ya kimataifa na mamlaka ya Ufalme wa Denmark. Walionya kwamba jaribio lolote la kulazimisha nchi mshirika wa NATO litakiuka misingi ya kujitawala ambayo muungano huo unatetea.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean‑Noël Barrot, alisema alizungumza na Rubio ambaye alikana kabisa uwezekano wa Marekani kufanya operesheni kama ile ya Caracas dhidi ya Greenland. Alisisitiza kuwa kuna uungwaji mkono mkubwa nchini Marekani kwa uanachama wa NATO, ambao utaathirika ikiwa Marekani ingeonyesha uhasama kwa nchi mwanachama wa muungano huo.