Maafisa wamefungua njia salama kwa raia kuondoka, ikiwa ni siku ya pili ya machafuko kati ya serikali na vikosi vya Kikurdi.
Serikali ya mkoa wa Aleppo iliwapa wakaazi muda hadi saa saba mchana majira ya Syria, ili waweze kuondoka kwa ushirikiano na jeshi. Likinukuu jeshi, shirika la habari linalomilikiwa na serikali SANA, limesema jeshi litaanza ‘operesheni maalum’ dhidi ya vikosi vya Syria Democratic (SDF) vinavyoongozwa na Wakurdi. Na kwamba baada ya muda huo, wangeanza kushambulia maeneo lililoorodhesha ikiwemo Sheikh Maqsoud, Achrafieh na Bani Zaid.
Mwandishi Habari wa Associated Press aliyeko Aleppo ameripoti kusikia milio ya mashambulizi huku raia wakimiminika nje ya mji asubuhi ya Alhamisi. Kufikia Jumatano, zaidi ya watu 46,000 walikuwa wamekimbia makaazi yao mkoani humo. Hayo ni kulingana na ofisi inayohusika na masuala ya Raia na Kazi ya Aleppo.
Kufuatia machafuko hayo yaliyoanza Jumanne, vikosi vya SDF vimesema kwamba takriban watu wanane wameuawa katika mitaa ambako wakaazi wengi ni wa Kikurdi. Nao maafisa wa serikali wameripoti vifo vya angalau raia watano na mwanajeshi katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali. Makumi ya watu kutoka pande zote mbili wamejeruhiwa.
Mohammad Ali ni Afisa Mtendaji wa Operesheni katika shirika la kutoa misaada White Helmets mjini Aleppo amewaambia waandishi habari kwamba “idadi kubwa ya watu wameondoka Alhamisi, takriban 11,000. Miongoni mwao, kuna asilimia kubwa wanaokabiliwa na changamoto kubwa za matibabu wakiwemo wazee, kina mama na Watoto.”
Umoja wa Mataifa na wa Ulaya waelezea wasiwasi, maafa kwa raia
Umoja wa Ulaya umeelezea wasiwasi mkubwa kuhusu machafuko ambayo yameukumba mji huo wa Syria.
Msemaji wa Umoja wa UlayaAnouar El Anouni amezitaka pande zote mbili kujizuia, kuwalinda raia na kusaka njia za kidiplomasia kutatua mzozo wao.
Mkuu wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen pamoja na rais wa kamisheni ya umoja huo Antonio Costa, wanatarajiwa kuzuru Damascus kwa mazungumzo na uongozi wa nchi hiyo.
Umoja wa Mataifa pia umeelezea wasiwasi wake kutokana na machafuko hayo.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric amewaambia waandishi Habari kwamba Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, anasikitishwa na ripoti za vifo vya raia na majeruhi kufuatia uhasama unaoendelea Aleppo.
Ametoa wito kwa pande zote husika kusitisha mashambulizi mara moja na kuchukua hatua zote za kuzuia maafa zaidi ya raia na warudi kwenye meza ya mazungumzo ili kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa Machi 10.
Kila upande unaulaumu mwingine kwa kushambulia makaazi ya raia kiholela na miundombinu.
Mkwamo katika utekelezaji makubaliano
Machafuko hayo yanajiri mnamo wakati kuna mkwamo wa kisiasa katika mazungumzo kati ya serikali na SDF.
Mnamo mwezi Machi, serikali ya Damascus ilisaini makubaliano na SDF inayodhibiti kaskazini mashariki, kwamba vikosi vyake viungane na jeshi la Syria ifikapo mwisho wa mwaka 2025. Lakini kumekuwa na kutofautiana jinsi hilo linaweza kutekelezwa.
APA, AFPE