Hati ya rais iliyosainiwa Jumatano na Trump, inazielekeza idara, taasisi na mashirika ya serikali ya Marekani kusitisha ushiriki wake na ufadhili kwenye mashirika 31 ya Umoja wa Mataifa, pamoja na mashirika mengine 35 yasiyo ya Umoja wa Mataifa haraka iwezekanavyo.
Kulingana na Ikulu ya White House, mashirika hayo yanafanya kazi kinyume na maslahi ya kitaifa, usalama, ustawi wa kiuchumi, au uhuru wa Marekani.#
Sera ya ”Amerika Kwanza” imezingatiwa
Ikulu ya Marekani, imesema uamuzi huu, ni sehemu ya mkakati wake wa “Amerika Kwanza” unaolenga kulinda maslahi ya kitaifa ya Marekani, hata kama hatua hiyo inaibua mjadala mkali duniani.
Taarifa ya Ikulu ya White House imeeleza kuwa Rais Trump anaachana na ushiriki wa Marekani katika mashirika ya kimataifa ambayo yanadhoofisha uhuru wa Marekani, na kupoteza dola za walipa kodi katika ajenda zisizofaa au zenye mrengo wa uadui.
Miongoni mwa mashirika yaliyoathiriwa ni yale yanayojihusisha na masuala ya mazingira, mabadiliko ya tabianchi na usawa wa kijinsia.
Orodha hiyo inajumuisha Jopo la Serikali Mbalimbali kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, IPCC, pamoja na Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, UNFCCC, ambao ndio msingi wa makubaliano makubwa ya kimataifa ya tabianchi.
Mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa yaliyoko kwenye orodha ni Shirika la Wanawake, Shirika la Idadi ya Watu, UNFPA, Shirika la Maendeleo na Biashara, UNCTAD, Shirika la Mpango wa Makazi ya Watu, UN-Habitat, Ofisi ya Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu kwa ajili ya Watoto kwenye Mizozo ya Kivita, pamoja na Ofisi ya Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu kuhusu Unyanyasaji wa Kijinsia katika Migogoro.
Rubio: Marekani inajiondoa kwenye mashirika yasiyo na manufaa
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, amesema Marekani inajiondoa kwenye mashirika aliyoyataja kuwa ”yanayoipinga Marekani,” yasiyo na manufaa au yanayopoteza fedha za walipa kodi. Katika chapisho lake kwenye mtandao wa kijamii wa X, Rubio amesema kuwa mapitio ya mashirika mengine yanaendelea.
Hatua hii pia inaendeleza msimamo wa Trump wa kujiondoa kwenye mifumo ya ushirikiano wa kimataifa. Tangu arejee madarakani, Marekani tayari imejiondoa kwenye Shirika la Afya Duniani, WHO na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO. Trump anadai kuwa Marekani imekuwa ikibeba mzigo mkubwa wa kifedha bila kupata faida ya moja kwa moja.
Uamuzi huu umekosolewa vikali na wanaharakati wa mazingira na demokrasia, wakisema kujitoa kwa Marekani kwenye UNFCCC na IPCC ni pigo kubwa kwa juhudi za kimataifa za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha ushirikiano wa dunia. Wapo pia wanaohoji uhalali wa kisheria wa rais kujiondoa kwenye mikataba iliyoidhinishwa na Baraza la Seneti la Marekani.
Aidha, Umoja wa Ulaya umeelezea kusikitishwa kwake na uamuzi huo wa Marekani, na hasa kujiondoa katika mkataba muhimu wa mazingira wa UNFCCC.
Ulaya kuendelea kushirikiana na nchi nyingine kwenye mazingira
Hata hivyo, Kamishna wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia Mazingira, Wopke Hoekstra amesema Alhamisi kuwa Ulaya itaendelea kufanya kazi na mataifa mengine ili kukabiliana na ongezeko la joto duniani, licha ya Marekani kutangaza kujiondoa UNFCCC.
Wakati Ikulu ya White House ikisisitiza kuwa hatua hizi zinalenga kulinda uhuru na maslahi ya Marekani, athari zake kwa ushirikiano wa kimataifa na juhudi za pamoja za kukabiliana na changamoto za dunia zinaendelea kujadiliwa. Dunia sasa inasubiri kuona majibu ya Umoja wa Mataifa na hatua zitakazofuata katika mvutano huu wa kisera.
(DPA, AFP, Reuters)