Msemaji wa wizara ya mashauri ya kigeni ya Urusi Maria Zakharova amesema makubaliano yaliyofikiwa na Ukraine na washirika wake wa Ulaya ni ya kijeshi, hatari na ya uharibifu mkubwa. Ameonya kwamba kutumwa kwa kikosi hiki nchini Ukraine kutachukuliwa na Urusi kama mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Urusi. Amesema na hapa namnukuu ” Tamko jipya la kile kinachoitwa muungano wa utashi na utayari na utawala wa Kyiv kwa pamoja vinafanya mhimili wa vita” mwisho wa kumnukuu.
Kauli ya msemaji wa wizara ya mashauri ya kigeni ya Urusi imekuja baada ya washirika wa Ukraine kukutana mjini Paris mji mkuu wa Ufaransa wiki hii na kukubaliana juu ya kuweka uhakika wa usalama wa Ukraine hususan mji mkuu wa Kyiv. Ni mkakati ambao utatekelezwa kwa ushirika wa Marekani ambayo itatoa mfumo wa uchunguzi na ufuatialiji wa masuala ya usalama huku nchi za Ulaya zikituma kikosi cha pamoja. Hata hivyo hatua hii ya Ulaya kutuma kikosi chake nchini Ukraine utatekelezwa ikiwa tu mapigano baina ya Urusi na Ukraine yatakuwa yamesimamishwa kupitia mpango wa mazungumzo ya pande mbili.
Urusi inasema mipango hii ya nchi za Ulaya inajaribu kuweka kikomo cha matumaini ya kupatikana usalama wa Ukraine katika mzozo ambao unaelekea kumaliza kipindi cha miaka mine.
“Vikosi vyote na zana za kivita zitakazotumwa kutoka Ulaya kwenda Ukraine Urusi itazichukulia kama zinazolenga vituo vyetu vyote vya kijeshi” alisema Zakharov msemaji huyo wa wizara ya mashauri ya kigeni ya Urusi.
Akielezea msimamo wa serikali yake kuiunga mkono Ukraine kufuatia vita vyake na Urusi, Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez amekemea hatua zinazoshuhudiwa katika mizozo mingine inayoendelea duniani:
“Ni dhahiri kwamba tunaishi katika dunia mpya, dunia ambayo ina mambo mengi, yenye chuki zaidi, yenye utata zaidi. Dunia ambayo kanuni na sheria zilizowahi kuweka muingiliano wa amani duniani kwa miongo kadhaa, karibu hazina maana tena. Au angalau inahisi kwamba karibu hazina maana tena baada ya kile tulichokishuhudia siku chache zilizopita.”
Serikali ya Urusi siku zote imeonya mara nyingi kwamba haitakubali hata siku moja nchi za jumuiya ya NATO au vikosi vya nchi za Ulaya kutumwa nchini Ukraine na imeonya kuvishambulia mara moja vikosi hivyo endapo vitatumwa.
Katika mkutano wa Paris, Ufaransa, Uingereza, na washirika wao wengine wa Ulaya walisaini waraka wa pamoja wenye nia ya kutuma kikosi cha kijeshi nchini Ukraine baada ya kusitisha vita, ijapokuwa taarifa zaidi kuhusu yaliyomo kwenye waraka huo bado kufahamika wazi.
Zelensky akemea kitendo cha Urusi kuendelea kulikalia Donbass
Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine yeye amesema kwamba hajapata uhakika kutoka kwa washirika wake wa Ulaya kuhusu ni kwa namna gani wataingilia kati endapo Urusi itaongeza mashambulizi zaidi kwa nchi yake.
Amesema tatizo kubwa katika mzozo huu ni kitendo cha Urusi kuendelea kulikalia eneo la Donbass na majeshi ya Urusi kuendelea kudhibiti kituo kikubwa cha nyuklia cha Zaporizhzhia nchini Ukraine.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na waziri mkuu wa Uingereza Keir Stammer wamesema makubaliano hayo yataweka utaratibu halali wa vikosi vyao kudhibiti anga la Ukraine na ukanda wa mwambao wa maji ya upande wa Ukraine huku wakiimarisha taratibu uwezo wa jeshi la Ukraine kwa mstakabali wa baadaye.
Urusi ambayo ilianzisha mashambulizi kwa Ukraine mwezi Febuari mwaka 2022 imesema kwa mara nyingine tena kwamba mashambulizi yake nchini Ukraine ni kuzuia kuingiliwa kijeshi na mataifa ya jumuiya ya NATO na kuonya kwamba kamwe haitakubali majeshi ya nchi za Ulaya kuweka vituo vyao nchini Ukraine.