Baada ya kumalizika vita vya miaka mitano vya wenyewe kwa wenyewe tangu mwaka 2013 hadi 2018 usalama na amani kiasi imerejea katika nchi hiyo yenye wakazi milioni 5.5 lakini inayopatikana katika ukanda wa machafuko na mizozo isiyoisha.
Rais Archange Touadera ameshinda muhula huu baada ya mabadiliko ya katiba yaliyoidhinishwa mwaka 2023 kupitia kura ya maoni. Anaiongoza moja ya nchi maskini kulingana na takwimu za mashirika ya fedha ya kimataifa na ambayo hadi sasa inategemea kwa kiasi kikubwa misaada ya wahisani licha ya kuwa na utajiri wa raslimali ya madini kama urani, lithium, dhahabu, shaba na misitu mikubwa inayozalisha mbao zenye thamani kubwa.
Mathilde Tarif, mtafiti katika chuo kikuu cha Ghent nchini Ubelgiji anasema changamoto kubwa ya Rais Touadera itakuwa ni kuimarisha vikosi vyake vya usalama. Kwa upande aliwaambia waandishi wiki hii mjini Bangui mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya kati kwamba atatoa nafasi ya kutosha kwa makundi yenye silaha kwa ajili ya mazungumzo ya kina kuhusu usalama wa nchi hiyo.
CAR ni kituo muhimu kwa kundi la mamluki wa Urusi, Wagner
Fulbert Ngodji, ambaye ni mchambuzi wa siasa za kimataifa kutoka shirika la kimataifa la Crisis group amesema serikali awali ilitoa mafunzo ya kijeshi kwa wapiganaji wenye silaha lakini baadaye makundi hayo yalibadili msimamo na kuanza kuishambulia serikali.
Ametoa mfano wa mapigano ya hivi karibu baina ya jeshi la serikali na kundi la AAKG yaliyotokea kusini mashariki mwa nchi hiyo. Ameonya kwamba mapigano hayo yanaongezeka huku misaada ya kutoka wahisani wa kimataifa kwa Jamhuri ya Kati ikiendelea kupungua.
Jamhuri ya Afrika ya Kati imesalia kituo muhimu na cha mwisho kwa kundi la mamluki kutoka Urusi maarufu kama Wagner ambacho kwa muda sasa kimekuwa mshirika mkuu wa serikali ya Jamhuri ya Kati huku kundi hilo likiendelea kufurahia mikataba minono ya malipo na madini ya shaba na dhahabu.
Wapiganaji wa kundi la Wagner wamekuwa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati tangu mwaka 2018 baada ya Rais Touadera kuomba msaada wa ulinzi na kulisaidia jeshi la nchi yake suala ambalo limechangia kuwepo kwa usalama nchini humo.
Wadadisi wa masuala ya kiusalama na kisiasa wanasema kwa sasa serikali ya Jamhuri ya Kati inadhibiti asilimia 90 ya eneo la nchi nzima ikilinganisha na asilimia 80 ya eneo zima la nchi hiyo lililokuwa likidhibitiwa na wapiganaji wenye silaha mwaka 2021.
Washirika wa kimataifa wanaendelea kumiliki utajiri wa madini ya Bangui
Kwa upande mwingine lakini Mathilde Tarif, mtafiti katika chuo kikuu cha Ghent nchini Ubelgiji anasema sasa Rais Touadera atategemea kwa kiasi kikubwa ushirikiano wake na Rwanda, nchi ya Falme za kiarabu na Urusi ili kuendelea kulinda usalama wa utawala na nchi nzima ya Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Mtafiti huyu amesema kutokana na kuendelea kupungua kwa misaada ya kimataifa itakuwa vigumu pia kwa wahisani wa jadi kwa nchi hiyo kama mashirika ya umoja wa mataifa na umoja wa ulaya.
Hata hivyo umoja wa Falme za kiarabu tayari imefadhili uwanja mpya wa ndege katika mji mkuu Bangui na mradi wa umeme wa nishati ya jua maarufu kama Sakai 2.
Washirika wa kimataifa wanaendelea kumiliki utajiri wa madini ya nchi hiyo ikiwa ni pamoja na Ufaransa ambayo inamiliki vibali vya kuchimba madini ya urani huku kundi la wagner likimiliki vibali vya uchimbaji wa shaba tangu walipoingia nchini humo.
Hadi sasa Rais Touadera amevutia baadhi ya uwekezaji mpya mjini Bangui, huku tabaka la kisiasa na kiuchumi nchini humo likianza pia kuwekeza tena. Lakini alisema pia maeneo ya vijijini bado yako katika “hali ya kutisha” kwa upande wa miundombinu, upatikanaji wa maji, na usafi wa mazingira.
Zaid ya asilimia 70 ya wakazi wa Jamhuri ya Afrika ya kati wanaishi katika umaskini wa kupindukia na wengi hawana uwezo wa kulipia gharama za elimu.