Wapiganaji hao wa AFC/M23 wamedai kuwa idadi hiyo ya vifo imeongezeka kufuatia shambulizi lingine lililotokea tarehe 2 Januari mwaka huu, ambapo watu 6 walipoteza maisha na zaidi ya wengine 40 kujeruhiwa baada ya ndege isiyokuwa na rubani kulilenga jengo lililokuwa linakaliwa na raia katikati mwa mji wa Masisi.
Akiuhutubia umati wa familia za wahanga wakiwemo pia viongozi wa M23, Emmanuel Ndizeye kiongozi mkuu wa wilaya hiyo aliezea masikitiko yake huku majeneza yakiwasilishwa kwa mwendo wa taratibu kwenye uwanja huu wa michezo ambamo hafla hiyo ilifanyika.
“Watu wanalia ndugu zao waliofariki baada ya kushambuliwa na utawala wa Tshisekedi. kwa ujumla ni watu 22 lakini idadi hiyo inaweza kuongezeka. Utawala wa Tshisekedi upo mbali nasi lakini kwa sababu ya roho mbaya yake ndio maana tumekutana hapa hii leo ili kuwazika ndugu zetu.”
Vilio na nyimbo za huzuni ndivyo vilitawala katika ukumbi huu ambamo mamia ya wananchi baadhi ikiwa ni wale kutoka wilaya ya Masisi walihudhuria sherehe hizo za mazishi kwa huzuni kubwa. Mama huyu alimpoteza mwanawe katika shambulizi la droni kwenye kijiji jirani cha Nyabyondo kilometa 10 magharibi mwa mji wa masisi, anafafanua zaidi.
“Tulikuwa tunakula chakula tukiwa tumeketi, ghafla tukasikia mlipuko kwenye kijiji cha katale ilikua ni ndege iliyokuwa ikirusha mabomu. Saa chache baadaye nyumba iliyokuwa inakaliwa na raia ikapigwa na bomu kando na soko.”
Hali ya usalama inaendelea kuwa mbaya
Licha ya wananchi wa eneo hilo kuusifu utawala wa AFC/M23 lakini bado hali ya usalama imeendelea kuwa mbaya katika baadhi ya maeneo mkoani kivu kaskazini na kusini. Wakizituhumu nchi zenye nguvu zaidi duniani kwa kufumbia macho hali mbaya mashariki mwa Kongo, ombi la wakaazi hao ni upatikanaji wa amani katika eneo hili linaloyumbishwa na vita vya muda mrefu.
“Kila yoyote anayekuwa hapa kama vile wanaharakati wa haki za kibinadamu, mtutetee sababu kwetu masisi tunateseka sana. Tunachoihitaji ni usalama sababu makombora yamekuwa mengi sana.”
Tangu kuendelea kushuhudiwa kwa mashambulizi hayo, hofu imetawala eneo la kivu kaskazini linalokaliwa na kundi hilo la wapiganaji wa AFC/M23 kufuatia shambulio hili la hivi punde la anga. Desemba mwaka uliopita, FARDC ilifanya mashambulizi kadhaa ya anga yakilenga maeneo ya waasi katika mji wa Masisi.