
Vituo vya kurekebisha tabia na hospitali za afya ya akili katika Kaunti ya Mombasa vimeripoti ongezeko la wagonjwa wanaohusishwa moja kwa moja na matumizi mabaya ya muguka.
Amina Mohammed, msimamizi wa Mombasa Women Empowerment Centre, anasema wagonjwa wengi walioko chini ya uangalizi wao wameathiriwa na matumizi ya muda mrefu ya muguka.
“Tunapowachukua barabarani, mara nyingi tunawakuta na mafurushi ya muguka. Familia zao husema walianza kutafuna taratibu, kisha wakaanza kuchanganya na vitu vingine hadi afya ya akili ikaharibika.”
Taib Basheib, Mkurugenzi wa Reach Out Centre Trust, anasema tatizo la muguka ni kubwa zaidi kuliko linavyoonekana.“Kwa tathmini zetu, karibu asilimia 100 ya watumiaji wa muguka tunaokutana nao wako katika hali mbaya—wanaishi mitaani au wana matatizo makubwa ya akili, hasa vijana wa umri wa miaka 15 hadi 25.”
Madhara ya Kiafya
Madaktari wanaeleza kuwa muguka ina kemikali za cathinone na cathine, ambazo husababisha msisimko wa muda mfupi na hisia za furaha.
Jalab Ashraf, mtaalamu wa afya, anasema matumizi ya muda mrefu yana madhara makubwa:“Huathiri mdomo na meno, husababisha vidonda vya tumbo, kuvimbiwa, kukosa usingizi, wasiwasi na sonona. Kwa muda mrefu, inaweza kusababisha kupoteza akili au wazimu.
”Wataalamu wanaonya kuwa athari hizi huongeza mzigo mkubwa kwa mfumo wa afya ya umma, hasa katika maeneo yenye rasilimali chache.
Changamoto za Kisheria na Msimamo wa Bunge la Kaunti
Wachambuzi wa sera wanasema marufuku ya ngazi ya kaunti inaweza kukumbana na changamoto za kisheria, ikizingatiwa kuwa serikali kuu imetangaza muguka kuwa halali.
Hata hivyo, Katiba ya Kenya inaruhusu serikali za kaunti kuchukua hatua za kulinda afya ya umma ndani ya mipaka yao.
Frankline Makanga, diwani wa Wodi ya Chaani na mjumbe wa Kamati ya Afya katika Bunge la Kaunti ya Mombasa, anasema suala la muguka linapaswa kushughulikiwa kama dharura ya afya ya umma, si hoja ya kisiasa.
“Hili si suala la kufanya siasa. Kadri muda unavyosonga, vijana wetu wanazidi kuumia. Muguka inasababisha kukosa usingizi na inaathiri afya ya akili kwa njia nyingi,” anasema.
Anasema Bunge la Kaunti litaiomba idara husika kuandaa sera mahsusi kuhusu mazao na bidhaa zinazofaa kuuzwa ndani ya Mombasa, huku akitoa wito kwa Bunge la Taifa kuiondoa muguka kwenye orodha ya mazao ya biashara.
Mitazamo Tofauti ya Kiuchumi
Si wote wanaounga mkono marufuku hiyo. Githinji Tatu, mfanyabiashara wa muguka, anasema kudhibiti ni bora kuliko kupiga marufuku kabisa.
“Muguka iendelee kuuzwa lakini iwekwe sheria kali za kudhibiti. Marufuku si suluhisho, kwa sababu wengi wetu tunategemea biashara hii kwa riziki,” anasema.
Hitimisho
Kadri mjadala kuhusu mustakabali wa muguka unavyoendelea, athari zake kwa vijana, familia na mfumo wa afya zinazidi kujitokeza wazi.
Wataalamu wanakubaliana kuwa tiba ya uraibu ipo, lakini wanasisitiza umuhimu wa kuwekeza katika elimu ya umma, kinga na sera shirikishi zitakazoweka afya ya jamii mbele ya maslahi ya kisiasa na kiuchumi.Swali linalosalia ni iwapo hatua za serikali ya kaunti zitafanikiwa kulinda afya ya vijana—au kama mgongano wa kisera kati ya kaunti na serikali kuu utaendelea kudhoofisha juhudi za kukabiliana na tatizo hili.