Maandamano hayo yalijitokeza katikati ya mvutano ulioongezeka baada ya utawala wa Rais Donald Trump kupeleka maafisa na mawakala 2,000 Minnesota kwa ajili ya msako mpya wa wahamiaji.
Mauaji ya Renee Good mwenye umri wa miaka 37 siku ya Jumatano yalisababisha mvutano kati ya maafisa wa shirikisho na wa jimbo kuhusu iwapo tukio hilo lilionekana kuwa la haki na iwapo wakala wa utekelezaji wa sheria wa Minnesota una mamlaka ya kulichunguza. Kumekuwa na taarifa zenye utata kuhusu namna tukio lenyewe lilivyotokea.
JD Vance: Mimi na Rais Trump tuko pamoja na ICE
Mapema Alhamis akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mkutano wa Ikulu ya White House, Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance amesema kuwa yeye na Rais Trump ‘wamesimama na ICE’ na kudai kuwa mwanamke aliyeuawa alikuwa ‘sehemu ya mtandao mpana wa mrengo wa kushoto wa kushambulia, kufichua taarifa binafsi na kufanya iwe vigumu kwa maafisa wao wa ICE kutekeleza majukumu yao’, madai ambayo hayajathibitishwa.
Katika nukuu yake amesema “Kwa sababu hili lilikuwa shambulio dhidi ya utekelezaji wa sheria za shirikisho. Hili lilikuwa ni shambulio dhidi ya sheria na utaratibu. Hili lilikuwa ni shambulio dhidi ya wananchi wa Marekani. Namna ambavyo vyombo vya habari, kwa ujumla, vimeripoti habari hii ni fedheha kabisa. Na inawaweka maafisa wetu wa usimamizi wa sheria hatarini kila siku.” Alisema kiongozi huyo.
Vance aliongeza kuwa afisa wa ICE aliyempiga risasi na kumuua mwanamke huyo aliwahi kuburuzwa na gari na kujeruhiwa. Na akisema kuwa afisa huyo ‘karibu apoteze maisha yake’ baada ya tukio hilo lililotokea miezi sita iliyopita, na kujeruhiwa vibaya kiasi cha kuhitaji kushonwa zaidi ya nyuzi 30 kwenye mguu wake.”
Namna tukio la mauwaji lilivyotokea
Mwanamke huyo alipigwa risasi akiwa ndani ya gari lake huko kusini mwa katikati ya jiji la Minneapolis, takriban kilomita 1.6 kutoka mahali ambapo polisi walimuua George Floyd mwaka 2020.
Video zilizorekodiwa na mashuhuda na kusambazwa mtandaoni zinaonyesha afisa akikaribia gari lililosimama katikati ya barabara, akimtaka dereva afungue mlango na kushika kitasa cha mlango. Gari aina ya Honda Pilot lilianza kusogea mbele na afisa mwingine wa ICE aliyesimama mbele ya gari hilo anatoa bastola na mara moja kafyatua angalau risasi mbili kwa umbali mfupi.
Hata hivyo haikuweza kujulikana mara moja kilichotokea kabla ya tukio la kufyatua risasi. Lakini Waziri wa Usalama wa Ndani Kristi Noem amesema maafisa walikuwa wanaikwamua gari yao moja iliokwama kwenye theluji na walikuwa wakiondoka eneo hilo wakati mvutano na tukio lilipotokea.
Rekodi nchini Marekani zinaonesha mauaji ya Good ni takriban kifo cha tano kinachotokana na msako mkali wa wahamiaji wa nchini humo ulionazishwa na utawala wa Trump mwaka jana.