
Jeshi la Syria limesema leo Jumamosi kwamba limefanikiwa kukamilisha udhibiti wa kiusalama katika eneo la Sheikh Maqsud katika mji wa Aleppo ambapo lilipambana na vikosi vya Wakurdi, ambalo hata hivyo limekana kupoteza udhibiti wa eneo hilo baada ya kukataa wito wa kujisalimisha.
Mashambulizi hayo ya vikosi vya serikali yamefanyika usiku kucha katika eneo hilo la Sheikh Maqsud baada ya muda wa mwisho uliowekwa kwa wapiganaji wa Kikurdi kusitisha mapigano na kujiondoa katika eneo hilo kupita.
Waandishi wa habari wa shirika la habari la AFP huko Aleppo wameripoti kwamba milio ya risasi katika eneo hilo la mwisho ambalo bado lilikuwa mikononi mwa Wakurdi imeendelea kusikika hadi asubuhi ya leo.
Tangu mapigano yaanze siku ya Jumanne, takribani watu 21 wameuawa, kulingana na takwimu kutoka pande zote mbili, na makumi ya maelfu wameukimbia mji wa Aleppo.