Kuelekea uchaguzi mkuu wa Januari 15 ncini Uganda, hali ya wasiwasi ni kubwa: magari ya kijeshi na wanajeshi kwa sasa yanatawala mandhari ya barabara katika mji mkuu Kampala, na Waganda wengi wana mashaka kuhusu uendeshaji wa mchakato huo. Uganda haijawahi kushuhudia mabadiliko ya madaraka kwa njia ya amani tangu kupata uhuru mwaka 1962.
Wananchi wanaisubiri siku ya uchaguzi kwa hofu, kama anavyosema Maria Taremwa: “Watu wanapigwa mitaani, hasa wapinzani.” Anasema agizo la kuwataka wapiga kura kuondoka kwenye vituo mara baada ya kupiga kura linaweza kuongeza mvutano. “Wengi wanataka kulinda kura zao—hilo linaeleweka, lakini linaweza kusababisha machafuko kwa urahisi.” Pia ana wasiwasi kuhusu uwezekano wa kuzimwa kwa mtandao: “Facebook imewekewa vikwazo tangu uchaguzi uliopita. Hilo linazuia uhuru wetu wa maoni.”
Jacob Nuwashumbusha—pia mkazi wa Kampala—anaonya kuhusu hatari ya hali kuchacha: “Kwa kawaida nisingetarajia mlipuko wa vurugu, lakini tumekalia juu ya pipa la baruti. Viongozi wa kisiasa wanapaswa kuwahimiza wafuasi wao kubaki watulivu.”
Yoweri Museveni — mkongwe madarakani
Rais Yoweri Kaguta Museveni anagombea tena muhula mwingine. Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 81 amekuwa madarakani tangu 1986 na analenga muhula wake wa saba. Hili limewezekana kupitia mabadiliko ya katiba aliyoyasimamia, yaliyofuta ukomo wa umri na mihula ya urais.
Museveni anajitambulisha kama mdhamini wa uthabiti. Katika hotuba ya Mwaka Mpya, alitetea msimamo mkali wa vyombo vya usalama na kuita matumizi ya gesi ya machozi dhidi ya “upinzani wa kihalifu” kuwa “halali na yasiyo ya kuua.”
Mpinzani wake mkuu ni Robert Kyagulanyi Ssentamu, anayejulikana kama Bobi Wine. Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 43 na mwenyekiti wa chama cha National Unity Platform (NUP) anawavutia hasa wapiga kura vijana.
Katika kampeni alisema uchaguzi huu “si uchaguzi mwingine tu, ni mapinduzi.” Tayari mwaka 2021 alijitokeza kama tumaini la kizazi kipya na, kwa mujibu wa matokeo rasmi, alipata takriban asilimia 35 ya kura—lakini uchaguzi huo ulikuwa na utata.
Hakuna imani kwa Tume ya Uchaguzi
Museveni na Bobi Wine ni miongoni mwa wagombea wanane waliokubaliwa kuwania kiti cha rais. Wapinzani wengine maarufu kama Kizza Besigye wamezuiwa na vifungo au mashtaka. Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi, takriban wapiga kura milioni 21.6 wamesajiliwa kwa mwaka 2026.
Mashaka kuhusu uhuru wa taasisi yameenea. Mwanasayansi wa siasa Frederick Golooba-Mutebi anasema: “Kuna mashaka kama uchaguzi utakuwa huru na wa haki. Uadilifu wa Tume ya Uchaguzi unatiliwa mashaka sana. Karibu kila uchaguzi nchini Uganda umeandamana na tuhuma za udanganyifu dhidi ya serikali na Tume ya Uchaguzi. Huu huenda ukaonekana vivyo hivyo.”
“Jeshi limehodhi uchaguzi”
Kampeni zimegubikwa na tuhuma za vurugu. Video zinaonyesha Bobi Wine akiwa amevaa mavazi ya kujikinga, na pia kuna picha za mashambulizi dhidi ya waandishi wa habari.
Shirika la haki za binadamua la Amnesty International linazungumzia “kampeni ya kikatili ya ukandamizaji” na limerekodi matumizi ya gesi ya machozi, kukamatwa na unyanyasaji wa wapinzani.
Pia kuna madai ya mateso na vifungo vya kiholela. Akizungumza na Shirika la Habari la Associated Press, Bobi Wine alisema kwamba “jeshi limechukua kwa kiasi kikubwa usimamizi wa uchaguzi.” Takribani wafuasi wake watatu wameripotiwa kuuawa.
Serikali inakanusha tuhuma hizo. Museveni alisisitiza kuwa uthabiti na maendeleo huenda sambamba na kwamba amani inapaswa kupewa kipaumbele ili Uganda iendelee kusonga mbele. “Mmeona kwa macho yenu mapigano nchini DR Kongo. Hamwezi kuchezea amani na usalama wetu kwa kumpigia kura mtu mwingine.”
Mwanasiasa Golooba-Mutebi anaona kukanusha huko hakushawishi: “Kila Muganda mwenye mtazamo wa haki ambaye amefuatilia kampeni hizi—bila kujali anaunga mkono chama gani—atakubali kuwa kampeni zimejaa vurugu.”
Anaongeza kuwa walioathirika zaidi ni wafuasi wa NUP: “Mara nyingi yalikuwa mashambulizi yasiyo na sababu.” Hata hivyo, vurugu zimekuwa sehemu ya kampeni kwa miongo kadhaa: “Tangu Rais Museveni alipojitokeza kugombea kwa mara ya kwanza mwaka 1995, kampeni za uchaguzi nchini Uganda zimekuwa zikifuatana na vurugu.”
Karibu na siku ya uchaguzi, hali inaweza kuzidi kuwa mbaya. Siku chache zilizopita, mamlaka zilipiga marufuku matangazo ya moja kwa moja ya machafuko. Bobi Wine alionya kuwa mtandao unaweza kuzimwa ili kuzuia uhamasishaji, lakini serikali inapinga. “Kwa sasa hakuna uamuzi wa kuzima mtandao,” alisema Nyombi Thembo wa Tume ya Mawasiliano ya Uganda.
Ni nafasi zipi za mabadiliko?
Mchambuzi Adolf Mbaine anaona ushindi mwingine wa Museveni kuwa na uwezekano mkubwa: “Anadhibiti vyombo vya usalama, anateua Tume ya Uchaguzi. Pia anaendesha kampeni nzuri.” Aidha, anafaidika na mafanikio fulani ya utawala wake. Chini ya hali hizi, mabadiliko ya madaraka yanaonekana kuwa magumu, anasema Mbaine. Ili kuwa na nafasi nzuri, upinzani ungehitaji kuungana na kusimamisha mgombea mmoja.
Golooba-Mutebi pia ana mashaka kuhusu mabadiliko baada ya uchaguzi: “Mabadiliko ya kweli yangemaanisha ama serikali mpya au muundo tofauti kabisa wa chama tawala cha sasa—hilo halina uwezekano mkubwa.” Anatumaini tu kwamba licha ya mvutano, vurugu na machafuko vitaepukwa baada ya uchaguzi.
“Katika hali bora, Museveni anashinda na mambo yanaendelea kama kawaida. Katika hali mbaya zaidi, Museveni anashinda, kunakuwa na pingamizi, mali zinaharibiwa na watu wengi wanauawa—hilo hakuna anayetaka.”
